NA MARYAM HASSAN

MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP), amewapandisha katika mahakama mbali mbali washitakiwa wa makosa ya udhalilishaji.

Yalijiri hayo katika mahakama ya mkoa Vuga, baada ya kijana Ali Suleiman Ali (29) mkaazi wa Magogoni, kufikishwa mahakamani hapo kwa tuhuma za kubaka.

Mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Makame Mshamba na kusomewa shitaka lake na wakili wa serikali, kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Fatma Saleh.

Wakili huyo alidai kuwa, mshitakiwa alitenda kosa hilo April 23 mwaka jana majira ya saa 4:00 za usiku huko Mwanakwerekwe wilaya ya Magharibi ‘B’ mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mshitakiwa alidaiwa kumuingilia katika sehemu za mbele mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 17 ambae si mke wake, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Mara baada ya kusomewa shitaka hilo, mshitakiwa huyo alikataa na kuiomba mahakama kumpa dhamana, jambo ambalo lilikataliwa na upande wa mashitaka.

Fatma alieleza kuwa, kosa aliloshitakiwa nalo mshitakiwa halina dhamana na badala yake kesi iahirishwe na kupangwa tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi.

Hakimu Makame alikubaliana na upande wa mashitaka juu ya kuahirisha shauri hilo na kuamua kuanza kusikilizwa ushahidi Januari 20 mwaka huu.

Pia ameamuru mshitakiwa kupelekwa rumande kwa kuwa kosa lake halina dhamana.