NA KHAMISUU ABDALLAH

MAHAKAMA ya mwanzo Mwanakwerekwe, imemuhukumu kulipa faini ya shilingi 200,000 mshitakiwa Mahir Mohammed Mashauri (22) mkaazi wa Kisauni.

Mshitakiwa huyo alitozwa faini hiyo na Hakimu Mohammed Ali Haji, baada ya kukubali kosa lake la kuendesha chombo cha moto bila ya hadhari na uangalifu.

Hata hivyo mahakama hiyo imefahamisha kwamba, endapo akishindwakulipa faini hiyo, atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi sita.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mohammed alisema, mahakama inamuona mshitakiwa huyo ni mkosa kisheria na kumpa adhabu hiyo, ili iwe fundisho kwake na madereva wengine.

Mshitakiwa huyo alilipa faini hiyo ili kujinusuru kwenda jela kwa muda huo.

Mahir, alifikishwa mahakamani hapo Januri 4 mwaka huu na kushitakiwa kwa kosa la kuendesha chombo cha moto bila ya hadhari na uangalifu, kinyume na kifungu cha 117 (1) cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.

Ilidaiwa kuwa, Agosti 4 mwaka 2018 saa 4:00 asubuhi huko Kisauni, akiwa dereva wa gari yenye namba za usajili Z 826 GN P/V akitokea Mbuyu Mnene kuelekea Maungani, alipofika Kisauni aliendesha gari hiyo bila ya hadhari na uangalifu na kupinda kwa ajili ya kurudi alikotokea katika sehemu isiyo ruhusiwa (U-Turn).

Mwendesha Mashitaka, Koplo wa Polisi Salum Ali alidai kuwa, kitendo hicho kilipelekea kumgonga mwendesha Vespa yenye namba za usajili Z 621 GS alietambulika kwa jina la Suleiman Mohammed Rashid, ambae alikuwa akitokea Kisauni kuelekea Mbuyu mnene na kupelekea kuvunjika mguu wake wa kulia na kupata maumivu mwilini mwake.