TEHRAN,IRAN

IRAN imeliambia shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya nyuklia kwamba inaimarisha utafiti katika kutengeneza vyuma vya urani, hatua ambayo itakuwa ukiukaji mpya wa viwango vilivyowekwa kulingana na mkataba wa mwaka 2015 wa nyuklia uliosainiwa na nchi zenye nguvu duniani.

Iran ilisema utafiti wao unakusudia kuzalisha mafuta ya hali ya juu kutumiwa kwenye mtambo wa utafiti ulioko Tehran.

Shirika la nishati ya atomiki (IAEA) lenye makao yake mjini Vienna limesema kupitia taarifa kwamba Iran imeliarifu kupitia barua kwamba hatua yake hiyo ni kufanyia marekebisho na ufanikishaji wa vifaa vinavyohusika kwa shughuli hizo, tayari imeanza.

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa Kazem Gharib Abadi alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba katika hatua ya kwanza, urani asilia itatumika kutengeneza chuma cha urani.