NA KHAMISUU ABDALLAH

KUTOFIKISHWA kwa mashahidi kwenye kesi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, iliyokuwa ikimkabili mshitakiwa Ali Ramadhan Salum (45) mkaazi wa Chuini wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, imeisababishia mahakama kuliondoa shauri hilo.

Hakimu Taki Abdalla Habib wa mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe, aliliondoa shauri hilo baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha kosa na kuamuru mshitakiwa huyo kuachiwa huru, chini ya kifungu cha 219 cha sheria namba 7 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar.

Kabla ya mahakama kutoa uamuzi huo, upande wa mashitaka uliokuwa ukiongozwa na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Soud Said.

Uliiambia mahakama kuwa upande wa mashitaka tayari umeshamaliza kuwasilisha mashahidi wanne, mahakamani hapo na mshitakiwa ameshamaliza kujitetea.

Mshitakiwa huyo awali alikuwa akikabiliwa na shitaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kinyume na kifungu cha 307 cha sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar.

Alidaiwa kuwa Oktoba 2 mwaka 2009 saa 11:00 jioni huko Chuini, kwa njia ya udanganyifu alijipatia fedha taslimu shilingi 2,400,000 kwa lengo la kumuuzia kiwanja Seif Suleiman Seif, huku akijua kwamba hana uwezo huo.

Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo kwa mara ya mwanza Januari 31 mwaka 2019 alilikataa, ndipo upande wa mashitaka ulipodai kuwa upelelezi wake tayari umeshakamilika.