WANANCHI wa Zanzibar na Watazania kwa ujumla leo wanasherekea kutimiza miaka 57 tangu kuasisiwa kwa Mapinduzi matukufu tarehe kama leo mwaka 1964.

Tangu Januari mosi mwaka huu, kumekuwa na shamrashamra mbali mbali za kuadhimisha kilele cha sherehe za Mapinduzi ikiwa ni pamoja na uwekaji wa mawe ya msingi na uzinduzi wa miradi ya maendeleo katika maeneo mbali mbali na shughuli za usafi wa mazingira.

Dhana ya kwanza ya kufanyika kwa Mapinduzi ni kuwasogezea wananchi huduma za kijamii na kimaendeleo kuwa karibu na maeneo wanayoishi jambo ambalo lilishindikana wakati wa utawala wa kiimla wa Kisultani.

Kwa mfano, chini ya utawala wa Sultani suala la elimu ilikuwa ikitolewa kwa matabaka na kwamba wale waliokuwa na hadhi katika jamii ndio waliokuwa wakifadika na elimu kuliko wale waliokuwa na hadhi ya chini.

Hali hiyo imebadilika sana kwani hivi sasa elimu haitolewi kulingana na matabaka ama hali za watu katika jamii, ambapo mtoto kutoka eneo lolote lile anaweza kusoma bure kwa ukomo na upeo wake kuanzisha chekechea hadi elimu ya juu.

Kitu cha kufurahisha zaidi ni kwamba tangu kuasisiwa kwa mapinduzi hayo, Zanzibar inasonga mbele kimaendeleo katika upatikanaji wa huduma za jamii, kwa mfano, hivi sasa Zanzibar huhitaji kutembea zaidi ya kilomita tano bila kukutana na kituo cha afya.

Aidha, maji safi na salama yamesambazwa na kuenezwa katika kila miji na vijiji tena yanapatikana bila usumbufu, huku yale maeneo yenye changamoto zikipatiwa ufumbuzi.

Upatikanaji wa umeme kwa visiwa vyote vya Unguja na Pemba umekuwa wa uhakika zaidi, ambapo umeme huo hivi sasa takriban umesambazwa karibu kila kijiji na shehia za Zanzibar.

Kwenye suala la usambazaji umeme serikali imefikisha huduma hizo hadi kwenye visiwa vidogo vidogo amavyo tangu kuumbwa kwa dunia hakujawahi kufika umeme katika maeneo hayo.

Dhana ya pili ya kufanyika kwa mapinduzi ya mwaka 1964 ambayo leo kwa furaha na heshima kubwa tunatimiza miaka 57 ni kumletea Mzanzibari heshima, hadhi, utu wake na uwezo wa kufanya maamuzi kwa maslahi ya nchi yake.

Tunachotaka kusema ni kwamba kimsingi mapinduzi yametuletea uhuru kamili kama Wanzanzibari, uhuru ambao tulipaswa kuwa nao hasa ikiwemo suala zima la kujitawala na katika kujiamulia mambo wenyewe.

Kwa mfano masuala yanayowahusu Wazanzibari hivi sasa hayaamuliwa na familia ama ukoo moja, ambapo kabla ya mapinduzi, ni familia ya Kisultani tu  ndiyo iliyokuwa ikiwaamulia wananchi wa Zanzibar mustakbali wa maisha yao.

Ni mapinduzi tu na hakuna kitu chengine yaliyowapa Wazanzibari uwezo wa kujiamulia mambo wenyewe, kwa umoja wao kupitia matumizi ya vyombo vya uwakilishi kama Baraza la Wawakilishi na kwa upande wa Serikali, Baraza la Mapinduzi.

Mapinduzi haya ndiyo yaliyozika tofauti za kitabaka, ukabila, rangi na hata kukwezwa baadhi ya nasabu za watu tabia zilizokuwepo kabla ya Mapinduzi ambapo leo tunazungumza kama Wazanzibari bila ya kuwa na chembe ya dhambi hizo.

Ni vyema wananchi wa Zanzibar na wale wenye wasiwasi juu ya maana halisi ya ‘MAPINDUZI DAIMA’ kuwa ni mpango wa kuwafikishia maendeleo ya kijamii na kiuchumi wananchi wote katika nyanja zote bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

‘MAPINDUZI DAIMA’ yamekuja kuondosha matabaka, upendeleo, chuki, rangi na itikadi mambo ambayo hayakuwa ya msingi, na badala yake ni maendeleo kwa wote bila vikwazo.

Msisitizo wetu kwa jamii ni kuendelea kuyaunga mkono mapinduzi, kwani takriban katika kipindi cha miaka 57 iliyopita kwa kiasi kikubwa tumeweza kuvuna na kuyafaidi matunda ya mapinduzi kwa njia moja ama nyengine.

Vyovyote itakavyokuwa Zanzibar ni nchi yetu, italindwa na sisi wenyewe, lakini pia uzalendo na ukakamavu katika kuunga mkono utekelezaji wa mipango ya serikali ndiyo jambo litakalotufanya tusonge mbele zaidi kimaendeleo.

Matunda hayo ndiyo leo hii yanayotufanya tutembee kifua mbele, tukijinasibu na kijigamba kwa kusema ‘MAPINDUZI DAIMA’.