NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa serikali inaendelea kuchukua juhudi za kufufua uchumi, ambapo ukusanyaji mapato umeanza kuimarika.

Dk. Mwinyi alieleza hayo jana katika hotuba yake ya maadhimisho ya miaka 57 ya mapinduzi aliyoitoa kupitia vyombo vya habari, ikiwa ni sherehe zake za kwanza tokea achaguliwe kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Alisema makusanyo yameanza kuongezeka kutoka bilioni 22 mwezi wa Oktoba hadi kufikia bilioni 36.9 mwezi wa Disemba 2020, mapato yaliyokusanywa na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB).

Dk. Mwinyi alisema kuwa sekta ya utalii imeendelea kuimarika ambapo lengo lililowekwa la kupokea watalii 250,855 ifikapo Disemba 2020 baada ya kuzingatia mwenendo wa maradhi ya COVID 19, hadi Novemba 2020 jumla ya watalii 212,050 wameitembelea Zanzibar sawa na asilimia 85 ya makadirio.

Alisema serikali ya awamu ya nane itasimamia kwa karibu uratibu, utangazaji na uendelezaji wa sekta hiyo ili itoe mchango mkubwa zaidi kwa wananchi.

Alifahamisha kwamba tatizo lililojitokeza la kuchelewa kupatiwa wageni huduma wanapofika katika uwanja wa ndege linatafutiwa ufumbuzi ili kuwaondoshea usumbufu.

Alieleza kuwa alitamani sherehe za mwaka huu ziwe na shamrashamra kama ilivyozoeleka kutokana na umuhimu wake hata hivyo, imelazimika kuzifanya kwa namna tofauti kutokana na athari za ugonjwa wa corona.

Dk. Mwinyi alisema busara na hekima zimeelekeza kuwa fedha zilizopangwa kutumika kwa ajili ya sherehe hizo zielekezwe katika kuimarisha huduma za jamii ikiwemo afya, elimu na maji safi na salama.

Aidha, alisema kuwa kuna kila sababu za kuyaenzi mapinduzi kwa sababu ndicho chombo kilichowavusha wananchi wa Zanzibar katika dhoruba za kutawaliwa.

“Kwa mnasaba huu, leo (jana) ni siku muhimu sana katika historia ya Zanzibar, ambapo miaka 57 iliyopita, wakulima na wafanyakazi wanyonge walikataa madhila ya kubaguliwa”,alisema.

Alisisitiza kwamba inapoadhimishwa miaka 57, kuna wajibu wa kuwakumbuka na kuwashukuru wazee waasisi wa Chama Cha Afro-Shirazi, walioongozwa  na marehemu mzee Abeid Amani Karume.

Dk. Mwinyi alieleza haja ya kuendelea kuuenzi na kuuendeleza umoja na mshikamano uliopo ambao ndio siri kubwa ya kuendelea kuwepo kwa hali ya amani na utulivu yenye kuimarisha maendeleo.

Alieleza kwamba serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu au kikundi cha watu watakaojihusisha na vitendo vya kuvuruga amani ya nchi na kuwasihi wananchi kuendelea kuaminiana, kuheshimiana na kuvumiliana na kusahau tofauti zao.

Alisema kuwa serikali inatarajia kujenga hospitali kubwa ya rufaa na ya kufundishia katika eneo la Binguni, ambayo itakidhi mahitaji ya wataalamu, vifaa na uwezo wa kimiundombinu ambapo mchakato wa ujenzi umeshaanza.

Aidha, serikali itahakikisha sehemu zote ambazo hivi sasa zinakosa huduma za umeme na maji zinapata huduma hiyo kwa mujibu wa mahitaji ya wananchi pamoja na kufanya mapitio ya miradi yote ya maji na umeme Unguja na Pemba.

Aliitaka wizara ya Ardhi kushirikiana na wakuu wa wilaya na wakuu wa Mikoa kumaliza migogoro yote ya ardhi ifikapo mwisho mwa mwaka huu na hapendi kusikia kuna mwananchi analalamikia kudhulumiwa ardhi yake.

Dk. Mwinyi alisema kuwa serikali imeamua katika mwaka ujao wa fedha kuongeza uwezo wa bajeti ya wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ili iweze kuwahudumia vijana vizuri zaidi.

Sambamba na hayo, alisema kwamba serikali ipo kwenye mchakato wa ujenzi wa bandari kubwa ya kisasa katika eneo la Mangapwani, pamoja na jitihada hizo, usimamizi wa shughuli za bandari na viwanja vya ndege utaimarishwa.

Alisema kuwa Serikali imedhamiria kurejesha nidhamu ya kufanya kazi na kutokomeza mtindo wa kufanya kazi kwa mazoea na kujinufaisha  na kamwe watumishi wa umma wasisahau kuwa wao ni watumishi sio mabwana na  wawatumikie kwa ufanisi, uadilifu na kwa heshima wananchi huku wakitambua kuwa huo ndio wajibu wao.

Sambamba na hayo, Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuuendeleza na kuuimarisha Muungano.

Dk. Mwinyi alimpongeza Dk. John Magufuli  kwa jitihada zake za kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wake pamoja na kupambana na vitendo vya rushwa, ufisadi, uhujumu wa uchumi, dawa za kulevya na kuzilinda rasilimali za nchi.