NA KHAMISUU ABDALLAH

HAKIMU Asya Abdalla Ali wa mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe, amemwachilia huru Ratibu Ashkina Juma (18) mkaazi wa Bububu wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mahakama ilimuachia huru mshitakiwa huyo na kuonekana kwamba hana kesi ya kujibu, juu ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili za kujupatikana na dawa za kulevya.

Hakimu Asya alieleza kuwa mahakama inaifuta kesi hiyo chini ya kifungu cha 216, kutokana na mkinzano wa utambuzi wa kielelezo kinachoonyesha kama kakamatwa nacho mshitakiwa.

Hata hivyo, mahakama ilitoa haki ya rufaa ndani ya siku 30 kwa mtu yeyote ambae hakuridhika na uamuzi huo.

Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Nyasi Haji Kombo, alidai kuwa kesi hiyo ipo kwa ajili ya uamuzi mdogo (rulling).

Mshitakiwa huyo alikuwa akikabiliwa na tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya, kinyume na kifungu cha 16 (1) (a) cha sheria namba 9 ya mwaka 2009 sheria za Zanzibar.

Alidaiwa kuwa Disemba 7 mwaka 2019 saa 2:15 usiku huko Kidato, alipatikana na nyongo nane za majani makavu kila moja likiwa limezongozwa katika karatasi ya kaki, kitendo mabacho ni kosa kisheria.