ZASPOTI
ABDULHAMID Nasib Ibrahim ni mwanafunzi mtoto wa mchezo wa karate aina ya Shotokan ‘ZASHOKA’ aliyeitangaza Zanzibar katika mashindano ya kimataifa kwa kuchukua ubingwa kwa mara ya pili mfululizo mwaka 2019 na 2020.
Mashindano hayo hufanyika kila mwaka na kuzishirikisha nchi za Afrika Mashariki ambapo mwaka zilikuwa ni Burundi, Rwanda, Kenya,Tanzania Bara na Zanzibar.
Mwaka jana mashindano hayo yalishirikisha wanafunzi watoto wawili na kupata nafasi ya tatu kwa kufikia hatua ya nusu fainali.
Mwandishi wa makala hii anaelezea jinsi ya safari yake ya kujiunga na mchezo wa karate pamoja na mafanikio aliyoyapata na kuibua kipaji chake.
Abdulhamid alizaliwa tarehe 23 /8/ 2010 katika hospitali ya Mnazimmoja mjini Unguja ambapo elimu yake hadi sasa anasoma darasa la nne katika Skuli ya Alquwiyy Islamic.
Yeye ni mtoto wa pili katika familia ya Nasib Ibrahim na alianza safari yake ya michezo mwaka 2017 kwa kujiunga na Chama cha Mchezo wa Karate ‘ZASHOKA’ katika klabu ya Amani Modern Karate ( Amani Stadium ), lakini pia anapenda kucheza mpira wa miguu.
Aliwataja walimu waliomfundisha karate akiwemo Sensei Mbwana, Sensei Amani, Sensei Dulla, Sensei Amrani, pamoja na Sensei Kombo katika ukumbi wa judo Mwanakwerekwe Unguja.
Aliwataja wachezaji wa karate anaowahusudu akiwemo IP Man Donien Sensei Jerome pamoja na Sensei Amrani kutokana na ufundishaji wenye kiwango na kuwapa moyo licha ya kuwa mdogo katika kuinua vipaji vyao.
Alisema mafanikio aliyoyapata ni kuiletea heshima nchi yake ya Zanzibar kwa kupata medali mbili za dhahabu katika kipindi cha miaka miwili mfululizo, pamoja na mchezo huo unamjenga kiakili na kuwa mkakamavu muda wowote.
Hata hivyo, alisema, matarajio kuwa na chuo chake cha karate ili kusaidia kuibua wimbi la vipaji vya mchezo huo pamoja na kuwa mpiganaji bora wa karate barani Afrika na ulimwenguni kote.
Aidha, alisema, mchezo anaoukumbuka zaidi katika maisha yake siku ya fainali ya mashindano ya Afrika Mashariki mwaka 2019 kwani ndio mara yake ya kwanza kushinda mashindano ya kimataifa na kumshinda mwanafunzi wa Sensei Jeromi wa Tanzania Bara na kujinyakulia medali ya dhahabu.
“Ni siku ambayo siisahau katika maisha yangu mimi ni mdogo, lakini, napenda karate na nilifurahi kumshinda mwanafunzi mwenzangu wa Tanzania bara na kupata medali”, alisema.
Abdulhamid ameiomba serikali kuwafanyia ufumbuzi baadhi ya changamoto zinazoikabili chama ili kuendeleza karate na kupata wageni kutoka nchi mbali mbali kwa kutoa taaluma ya mchezo huo.
Hivyo aliwasahauri watoto wenzake kujiunga na karate ili kukuza ufahamu wa skuli pamoja na madrasa kwa ajili ya kupatikana wataalamu katika nchi.