NA MWANAJUMA MMANGA

MASHEHA wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ wametakiwa kushirikiana na wananchi wao ili waweze kupata taarifa za wananchi wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Aboud Hassan Mwinyi, aliyasema hayo katika kikao kazi na masheha wa wilaya hiyo kwa ajili ya kujitambulisha kilichofanyika ofisini kwake huko Mahonda na kueleza kuwa wanatakiwa kuhakikisha wanazuia uhalifu kabla haujatokea.

Alisema vitendo vya uchimbaji wa mchanga holela, uuzaji wa pombe, na uchinjaji wa ng’ombe bila ya kufuata sheria na taratibu ni mambo yanayoweza kuzuilika iwapo viongozi hao watakuwa karibu na wananchi wao lakini pia vyombo vyengine vya sheria.

Aboud alisema mashirikiano ya pamoja yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa vitendo hivyo katika jamii na kuwachukulia hatua za kisheria watendaji wa vitendo hivyo.

Alisema ili kukabiliana na vitendo vya kihalifu ni vyema wakabuni miradi itakayosaidia vijana kujiajiri na kuondokana na utegemezi ambao umekuwa ukisababisha kutokea kwa vitendo hivyo na kurudisha nyuma juhudi za wananchi katika kujikwamua kiuchumi.

“Niwaombe sana wananchi kujishughulisha na biashara yoyote ambayo ya halali itakayomsaidia yeye kujitafutia rizki na kuachana na kujishughulisha na biashara zisizoeleweka na zisizo rasmi,” alisema Aboud.

Akizungumzia tatizo la migogoro ya ardhi, Aboud aliwataka watendaji hao kutojihusisha na migogoro hiyo na badala yake waitafutie ufumbuzi kwa kushirikisha pande mbili na ikiwashinda waifikishe ngazi ya wilaya ili iweze kutatuliwa.

Hata hivyo amewataka masheha kutoa huduma bila ya upendeleo ili kila mwananchi aweze kupata haki yake kwa mujibu wa sheria na miongozo ya serikali inavyoelekeza.

Mapema wakitoa maelezo yao mbele ya Mkuu huyo wa wilaya masheha hao wamesema katika shehia zao wanakabiliwa na tatizo la ubovu wa mapaa ya skuli za Mgambo na Fujoni, Madai ya fedha kwa baadhi ya wananchi wa shehia ya kwa Gube waliouziwa viwanja na baraza la mji Kaskazini ‘B’.

Alisema pamoja na matatizo hayo lakini pia kuna tatizo la daraja katika shehia ya Mgambo hali ambayo inawapa wasiwasi wa kukosa mawasiliano katika kipindi cha mvua za masika.

Hata hivyo wameomba mamlaka husika kukumbushwa madai ya fidia za miti ya mazao kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara ya Kilombero, Mgonjoni, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Donge skuli hadi Chaani, pamoja na tatizo la uchomaji wa taka katika kituo cha afya Makoba.