ZURICH, Uswisi
KLABU ya Bayern Munich watamenyana na mabingwa wa Afrika, Al Ahly au Al Duhail ya Qatar katika nusu fainali ya Klabu Bingwa ya Dunia ujao, kufuatia ‘droo’ kwenye makao makuu ya FIFA huko Zurich juzi.

Nusu fainali hiyo itachezwa Jumatatu ya Februari 8 katika uwanja wa Ahmad Bin Ali huko Al Rayyan, nje kidogo ya mji mkuu wa Qatar, Doha.

Kabla ya hapo Al Ahly na Al Duhail watakutana Februari 4 katika Uwanja wa Education City, uwanja mwengine wa Kombe la Dunia la 2022 huko Qatar.


Miamba hiyo ya jijini Cairo, Al Ahly wanaofundishwa na Pitso Mosimane wa Afrika Kusini, ndiyo klabu iliyofanikiwa zaidi barani Afrika ikiwa mabingwa mara tisa.

Wakati huo huo, Al Duhail, ambayo meneja wake ni mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa na Rennes na kocha wa Nottingham Forest, Sabri Lamouchi, wamefuzu wakiwa mabingwa watetezi wa taifa hilo wenyeji.

Kwa upande mwengine wa ‘droo’, klabu ya Mexico, Tigres UANL, washindi wa Ligi ya Mabingwa ya CONCACAF, watachuana na mabingwa wa Asia, Ulsan Hyundai wa Korea Kusini mnamo Februari 4 na kwa haki ya kuwavaa washindi wa Copa Libertadores katika nusu fainali ya kwanza mnamo Februari 7.

Miamba ya Brazil ya Santos na Palmeiras watapambana kwenye mechi iliyocheleweshwa ya Marekani Kusini mjini Rio de Janeiro kwenye uwanja wa Maracana mnamo Januari 30.

Wabrazil wenzao wa Flamengo walipoteza fainali ya 2019 na Liverpool, na klabu za Ulaya zimekuwa zikishinda kila moja ya fainali saba za Klabu Bingwa ya Dunia.