CAIRO, Misri
KLABU ya Al Ain ya Emirates ina azma ya kumsaini mshambuliaji wa Zamalek, Ahmed Sayed Zizo katika dirisha la sasa la uhamisho wa msimu wa baridi.

Zizo amekuwa kipenzi cha mashabiki wa ‘weupe hao’ baada ya kucheza sehemu kubwa katika mafanikio ya Zamalek ndani ya Misri na michuano ya Afrika msimu uliopita.

Ushiriki wake wa magoli 17 kwa yoso huyo wenye umri wa miaka 24 [mabao tisa na usaidizi nane] uliiongoza Zamalek kwenye SuperCup ya CAF na ile ya Misri.
Kiwango chake kimezivutia klabu kadhaa, huku mahasimu wakubwa wa Zamalek, Al Ahly wakiripotiwa kupendezwa naye.

Wakala wa soka wa Misri, Nader Shawky, hapo awali alithibitisha kuwa klabu isiyojulikana ya Emirati ilianza mazungumzo na Zizo na sasa inaonekana kuwa ofa rasmi imewasilishwa.Kulingana na ripoti nchini Misri, Al Ain wametoa kwa ‘White Knights’ ya euro milioni 2.5 ili kupata huduma za nyota huyo wa zamani wa Moreirense.(Goal).