NA MARYAM HASSAN

HAKIMU wa mahakama ya wilaya Mwera, Rauhia Hassan Bakari, amemnyima dhamana mshitakiwa Suleiman Khamis Mgeni (30) mkaazi wa Amani Unguja, ambae alifikishwa mahakamani hapo kwa kosa wizi wa mazao.

Hakimu huyo, aliamuru mshitakiwa huyo kupelekwa rumande hadi Januari 11 mwaka huu kesi yake itakapoendelea kusikilizwa ushahidi.

Akiwa mahakamani hapo, Suleiman alisomewa shitaka lake na wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Sara Omar Hafidh.

Wakili huyo alisema, mshitakiwa alitenda tukio hilo Disemba 27 mwaka jana majira ya saa 8:20 usiku huko Uzini wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Mshitakiwa kwa njia ya kudanganya na bila ya kuwa na dai la haki, aliiba kuku watano majogoo kati ya hao watatu rangi nyeusi na majike wawili rangi ya udongo, wote wakiwa na thamani ya shilingi 75,000 mali ya Makame Haji Makame.

Mara baada ya kusomewa shitaka lake mshitakiwa huyo alikataa na badala yake, upande wa mashitaka uliwasilisha mashahidi wawili na  tayari wamesikilizwa.

Kwa kuwa Hakimu Rauhia aliahirisha shauri hilo, mshitakiwa alipelekwa rumande hadi Januari 11 mwaka huu.