NA HUSNA SHEHA

MAHAKAMA ya Mkoa Mahonda, imempeleka rumande kijana mmoja anaekabiliwa na tuhuma ya wizi wa mifugo.

Kijana huyo alitambulika kwa jina la Ali Khamis Juma (25) mkaazi wa Mahonda Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Mkoa wa Kaskazini Unguja,

Akisomewa shitaka lake na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Raghida Said Abdalla, mbele ya Hakimu Faraji Shomari Juma.

Mwendesha Mashitaka huyo alidai mahakamani hapo kuwa, mshitakiwa huyo aliiba ng’ombe mmoja jike mwenye rangi nyeusi akiwa na thamani ya shilingi 1,000,000 kwa makisio, ikiwa ni mali ya Mpemba Juma Mpemba.

Mshitakiwa huyo alidaiwa kufanya wizi huo Machi 30 mwaka jana muda usiofahamika, huko Kijini Matemwe Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyowasilishwa mahakamani hapo inadai kuwa, kutenda wizi wa mifugo ni kosa kisheria, kinyume na kifungu cha 259 (c) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.  

Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka lake alikataa, huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wa shauri hilo tayari umeshakamilika na kuomba kutolewa hati za wito kwa mashahidi.

Baada ya maelezo hayo ya upande wa mashitaka, mshitakiwa huyo aliiomba mahakama impatie dhamana, ombi ambalo lilikubaliwa pande zote mbili mahakamani hapo.

Hakimu Shomari, alimtaka mshitakiwa huyo kujidhamini kwa kima cha shilingi 1,000,000 na kuwasilisha wadhamini wawili ambao watasaini kwa kima kama hicho cha fedha, huku wakiwa na barua za Sheha wa Shehia wanazoishi pamoja na kuwasilisha vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi.

Hata hivyo, pamoja na kuiomba mahakama impatie dhamana mara baada ya kukana shitaka hilo, mshitakiwa huyo amejikuta akielekea rumande kwa muda wa wiki mbili, baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana aliopewa na mahakama. Kesi hiyo imeahirishwa na kutarajiwa kufikishwa tena mahakamani hapo Februari 2 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa mashahidi.