NA MARYAM HASSAN

SULTAN Omar Abdalla (19) mkaazi wa Sarayevo, amepelekwa rumande baada ya kunyimwa dhamana na mahakama ya mkoa Vuga, kwa makosa aliyoshitakiwa nayo ikiwemoa kosa la kubaka.

Mtuhumiwa huyo alipandishwa katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Salum Hassan Bakari, na kusomewa shitaka lake na Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Shamsi Yassin Saad.

Ilidaiwa kuwa, tukio hilo ametenda Novemba 6 mwaka jana majira ya saa 12:45 za jioni huko Sarayevo, wilaya ya Magharibi ‘B’ mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mtuhumiwa anadaiwa kumtorosha mtoto wa kike mwenye umri wa 14 (jina linahidhiwa).

Shamsi alidai kuwa, mbali na kumtorosha pia anadaiwa kumuingilia kimwili mtoto huyo ambae si mke wake, huku alijua kuwa jambo hilo ni kosa kisheria.

Mara baada ya kusomewa shitaka lake mshitakiwa huyo alikataa na kuiomba mahakama kumpa dhamana, jambo ambalo limekataliwa.

Kwa upande wa wakili huyo aliiomba mahakama kuahirisha shauri hilo na kupangwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi.

Pia alisemam katika kesi hiyo tayari upelelezi imekamilika hivyo kupangwa tarehe nyengine kutawapa nafasi ya kuwaita mashahidi katika kesi hiyo.

Hakimu Salum alikubaliana na upande wa mashitaka na kuamua kulitupilia mbali ombi la mshitakiwa na badala yake aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 11 mwaka huu, huku akiamuru mshitakiwa apelekwe rumande.