NA JOSEPH NGILISHO ARUSHA

KAMATI ya ushauri ya mkoa wa Arusha (RCC) imepitisha  zaidi ya bilioni  303 kama mapendekezo  ya mpango wa bajeti na makadirio ya mkoa wa Arusha kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Akisoma mapendekezo ya mpango wa bajeti hiyo, Jana Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega,  katika kikao cha kamati hiyo, alisema kuwa sekretariet ya mkoa imeanza rasmi mandalizi ya mpango wa bajeti ambao unahusisha hatua muhimu.

Alieleza kuwa utekelezaji wa bajeti ya mkoa 2021/2022 utazingatia vipaumbele vya mkoa ambavyo ni kuendelea na uimarishaji wa elimu ya msingi na sekondari katika ngazi zote kwa kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Maeneo mengine ni kuboresha huduma za afya ya kinga na tiba katika ngazi zote kupitia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya afya, kuimarisha upatikanaji wa dawa muhimu na vifaa tiba ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wa afya.

Alieleza kuwa vipaumbele vingine ni kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na maji taka kwa kujenga miundombinu mipya na kufanya ukarabati wa miundombinu iliyopo, kuimarisha pato la mkulima kwa kuongeza tija katika umarishaji wa mazao, kuongeza thamani ya mazao na kuimarisha mfumo wa huduma za ugani.

Alisema katika kuimarisha pato la mkulima pia wataendeleza kilimo cha umwagiliaji kwa kujenga na kukarabati mifumo ya umwagiliaji husan katika Bonde la Eyasi, kuimarisha miundombinu na utafutaji wa masoko pamoja na kuongeza matumizi ya pembejeo na zana bora za kilimo.

Kwa upande wa mifugo Kwitega alisema kuwa wataporesha afya za mifugo kwa njia ya chanjo dhidi ya maradhi, kuimarisha miunfombinu ya ufugaji, kuimarisha mazao ya mifugo na uvuvi pamoja na kutenga maeneo mahususi ya malisho kwa ajili ya wafugaji.

Alibainisha vipaumbele vingine kuwa  ni kuimarisha sekta ya viwanda kwa kutenga maeneo ya uanzishwaji wa viwanda na kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara, kuimarisha miundombinu ya utalii kwa kuhamasisha utalii wa ndani ukiwemo utalii wa mambo ya kale.

Pia alisema kuweka vivutio kwa watalii ili kuongeza siku za kufanya utalii mkoani Arusha pamoja na kuipatia ufumbuzi migogoro yote inayojitokeza kati ya wananchi na wanaoishi maeneo ya jirani na hifadhi na mamlaka husika.

Aidha alisema kuwa katika kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele hivyo mkoa unatarajia kutumia jumla ya shilingi bilioni 303,172,660,428 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo ambapo mishara ya watumishi ni 178,059,162,00 miradi ya maendeleo 71,041,303,428, matumizi mengineyo 11,480,490,000 pamoja na mapato ya ndani ya halmashauri 42,591,705,000.

Sambamba na hayo pia alieleza mchanganuo wa makadirio ya ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo halmashauri ya Arusha jiji inataraiwa kukusanya 22,099,965,000, Arusha DC 4,219,640,000, Karatu 4, 501,993,000, Longido DC 2,208,158,000, Meru DC 4, 049,395,000, Monduli 2,677,908,000 pamoja na Ngorongoro 2,834,646,000 jumla ikiwa ni Bilioni 42, 591,705,000 ambapo  mchango wa halmashauri kwenye miradi ya maendeo ni billioni 3,239,601,827