NA KHAMISUU ABDALLAH
DEREVA aliyedaiwa kuficha nambari za usajili katika chombo chake wakati akiwa anaendesha barabarani, ametozwa faini ya shilingi 30,000 au kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi mitatu.
Hakimu Amina Mohammed Makame wa mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe, alitoa adhabu hiyo kwa mshitakiwa Ali Kombo Bakar (26) mkaazi wa Kinuni wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, baada ya kukubali kosa lake aliposomewa mahakamani hapo.
Akitoa adhabu hiyo, alisema mahakama inamuona mshitakiwa huyo ni mkosa kisheria na kumpa adhabu ya kulipa faini hiyo na akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi mitatu.
Mshitakiwa huyo alilipa faini hiyo ili kujinusuru kwenda jela kwa muda huo.
Mapema Mwendesha Mashitaka wa mahakama hiyo Koplo wa Polisi, Salum Ali, alidai kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la kuendesha chombo cha moto ikiwa nambari za usajili nyuma amezificha, kinyume na kifungu cha 13 (a) sura ya 59/2007 na kifungu cha 201 (1) na kifungu cha 205 (2) (a) cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.
Mshitakiwa Ali alidaiwa kuwa, Disemba 22 mwaka jana majira ya saa 10:40 jioni akiwa dereva wa honda yenye namba za usajili Z 248 JU akitokea Koani kuelekea Mwembemchomeke, alipatikana akiendesha honda hiyo barabarani ikiwa namba za usajili za nyuma hazisomeki kwa kiziziba na kuzibenua juu, jambo ambalo ni kosa kisheria.