NA KHAMISUU ABDALLAH

DEREVA aliyedaiwa kuendesha honda ikiwa haina namba za usajili, ametozwa faini ya shilingi 200,000 katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe.

Talib Hijja Nassor (28) mkaazi wa Darajabovu, alitozwa faini hiyo na mahakama baada ya kukubali makosa yake ya usalama barabarani.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Suleiman Jecha Zidi alisema, kwa kosa la kuendesha chombo cha moto kikiwa hakina namba za usajili, mshitakiwa atalipa faini ya shilingi 180,000 na akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi mitatu na kosa la kutotii sheria za njia, kulipa faini ya shilingi 20,000 au kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa wiki moja.

Mshitakiwa huyo alilipa faini hiyo ili kujinusuru kwenda jela kwa muda huo.

Mwendesha Mashitaka wa Polisi Shahida Haji, alidai kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na makosa mawili ikiwemo la kuendesha chombo cha moto kikiwa hakina namba za usajili, kinyume na kifungu cha 27 (1) (3) cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.

Ilidaiwa kuwa Disemba 27 mwaka jana, saa 9:30 jioni huko Mwanakwerekwe sokoni akiwa anaendesha honda akiwa anatokea Mwanakwerekwe kwenye mzunguko wa barabara kuelekea Mwanakwerekwe makaburini, alipatikana akiendesha honda hiyo barabarani ikiwa haina namba kitendo ambcho ni kosa kisheria.

Aidha kosa jengine alilopatikana nalo mshitakiwa huyo ni kutotii sheria za njia, kinyume na kifungu cha 143 cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.

Mshitakiwa Talib, alidaiwa kuwa siku hiyo hiyo alipatikana akiwa amesimamisha honda yake katikati ya barabara na kusababisha msongamano kwa watumiaji wengine wa barabara hiyo, kitendo ambacho ni kosa kisheria.