NA MARYAM HASSAN

ALIYEDAIWA kumtorosha mtoto wa kike kutoka nyumbani kwao Ubago na kumpeleka vichakani, amepandishwa katika mahakama ya mkoa Mwera.

Mshitakiwa huyo ni Feysal Haji Kaiza (23) mkaazi wa Ubago wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja, amepandishwa katika mahakama ya mkoa Mwera mbele ya Hakimu Said Hemd Khalfani.

Akiwa mahakamani hapo, alisomewa shitaka lake na wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Sara Omar Hafidh.

Alidai kuwa, mshitakiwa alitenda kosa hilo Januari 1 mwaka jana majira saa 2:30 usiku huko Ubago wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Wakili huyo alieleza kuwa, mshitakiwa bila ya halali alimchukua mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 ambae bado yupo chini ya uangalizi wa wazazi wake na ambae hajaolewa, kutoka nyumbani kwao Ubago na kumpeleka vichakani huko huko ubago kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Mara baada ya kusomewa shitaka lake mshitakiwa huyo alikataa na kuiomba mahakama kumpa dhamana, jambo ambalo lilikubaliwa katika mahakama hiyo.

Sara alisema hana pingamizi juu ya kupewa dhamana mshitakiwa huyo kwa sababu kosa lake linadhaminika, lakini aliomba upande mahakama kutoa masharti madhubuti na yenye kutekelezeka.

Pia aliomba kuahirishwa kwa shari hilo na kupangwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi, kwa sababu upande wa mashitaka umeshakamilisha upelelezi.

Hakimu Khamis Ali Simai, alikubaliana na maelezo yaliyotolewa na upande wa mashitaka na kumtaka mshitakiwa kusaini bondi ya shilingi 500,000.

Pia alisema, mshitakiwa awasilishe wadhamini wawili ambao watasaini kima hicho hicho pamoja na barua ya Sheha na kopi ya kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.

Alisema kama mshitakiwa atakamilisha masharti hayo atakuwa nje hadi Janiari 11 mwaka huu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi, hali ambayo imepelekea kutimimiza masharti aliyopewa.