NA TATU MAKAME

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, amesema kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi na cheti cha kuzaliwa ni haki ya kila Mzanzibari hivyo atahakikisha kila mwenye sifa anapata haki hiyo.

Akizungumza na wananchi waliokwenda kufuatilia vyeti hivyo huko ofisi ya usajili wa matukio ya kijamii, wilaya ya Kaskazini ‘A’, Gamba Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa vyeti na vitambulisho hivyo wilayani humo kutokana na watu wengi hawana vitambulisho hivyo jambo ambalo limesababisha kuwa na foleni kubwa katika kituo hicho.

Alisema ili kuhakikisha kila mwananchi anapata haki hiyo kwa wakati, ameagiza kuongezwa kwa mashine inayohifadhi kumbukumbu pamoja na kuwasogeza karibu watoa huduma za malipo na mpiga picha.

“Hatua hizi zitasaidia kuwapunguzia usumbufu wananchi wa kupata huduma kila mtu aliyefikia umri basi atapatiwa haki yake,” alieleza Ayoub.

Aidha aliwataka wananchi hao kuendelea kuwa wastahamilivu wakati serikali ya mkoa ikitafuta ufumbuzi wa tatizo hilo lililodumu kwa muda mrefu mkoani humo.

Naye Ofisa Usajili wa Matukio ya Kijamii wa wilaya hiyo, Mussa Ussi Pandu, alikiri kuchelewa kupatikana kwa vyeti kutokana na uhaba wa vitendea kazi pamoja na wananchi wengi kukosa kumbukumbu za taarifa zao.

Nao baadhi ya wananchi waliofika katika ofisi hizo, walisema wanakwenda kufuatilia vitambulisho hivyo asubuhi na kuondoka jioni bila ya mafanikio jambo ambalo linasababisha kutokufanya shughuli zao nyengine za maendeleo.