COLOMBO, SRI LANKA
MKUU wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet ameitaka mahakama ya kimataifa ya jinai kufanya uchunguzi kuhusu mzozo wa jamii ya Watamil wanaotaka kujitenga Sri Lanka.
Mkuu huyo pia ameitaka mahakama hiyo kuwachunguza maofisa wa kijeshi wanaotuhumiwa kushiriki uhalifu wa kivita na ikibainika wamefanya jinai wanapaswa kuekewa vikwazo.
Shirika la habari la AFP, limemnukuu Bachelet ambapo lilisema mkuu huyo aliishutumu Sri Lanka kwa kutotimiza ahadi zake za kuhakikisha haki inatendwa kwa maelfu ya raia waliouawa katika awamu za mwisho za vita vya utengano vilivyodumu kwa miaka 37.
Kwenye ripoti hiyo, Bachelet alisema juhudi za kitaifa za uwajibishwaji na maridhiano mara kwa mara zimeshindwa kuzaa matunda.
Badala yake zinazidisha uvunjaji sheria wa kiholela na kuwafanya raia kutouamini zaidi mfumo wa serikali.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa serikali ya rais Gotabaya Rajapaksa imerudisha nyuma baadhi ya hatua zilizopigwa chini ya tawala zilizotangulia katika kulinda haki za raia.