PASINA shaka kukaribishwa uwekezaji malengo yake makuu ni kuimarisha mapato ya serikali, kuunda fursa za ajira na kukuza utaalamu, baada ya sekta za uzalishaji tulizozizoewa miaka nenda miaka rudi kuzidiwa.

Mipango hiyo haikuamuliwa kwa kubahatisha, bali mambo kadhaa wa kadhaa yalizingatiwa, ikiwa ni pamoja na uhalisia wa Zanzibar kuwa ni visiwa visivyokuwa na maliasili nyingi kama za baadhi ya nchi nyengine.

Nchi za wenzetu zimejaaliwa kuwa na fursa nyingi za kukuza uchumi na mipango ya uzalishaji, hizo ni nchi zenye utajiri wa madini, ardhi kubwa kwa ajili ya kilimo, wanyama, mito na maziwa makubwa.

Udogo wa ardhi ya Zanzibar unatufanya tuwe makini zaidi na kuelewa kwamba iwapo mipango na mikakati yetu itakuwa butu kwa kiasi kikubwa hatutaweza kupiga hatua na kuondokana na hali mbaya za kimaisha.

Hali tuliyonayo hivi sasa tutaondokana nayo endapo tutapiga kasi katika kupata wataalamu wazalendo wenye upeo mkubwa kutoka miongoni mwa vijana wetu wanaomaliza masomo yao.

Suala la msingi kabisa lazima tuwaandae wataalamu na wafanyakazi wazalendo kuwa majasiri kurithi ujuzi, maarifa na hata teknolojia inayoletwa na wageni wanaowekeza au kupewa zabuni za miradi mkubwa.

Nchi nyingi za Asia ambazo zimeweza kupiga hatua kubwa na kuondoka katika kundi la mataifa yaliyozongwa na umasikini maarufu kwa jina la ‘Asian Tigers’, zilikaribisha wawekezaji au kutoa zabuni kwa wageni, lakini zilihakikisha ujuzi wao wanaupata wazalendo.

Kwa Mahathir Mohamed, waziri Mkuu wa muda mrefu wa Malasyia amewahi kusema kuwa wageni wanaonufaika na miradi katika nchi, halafu wanaondoka na kuziachia madeni, badala ya ujuzi nchi husika hawana faida kwa nchi hizo.

Kwa maana hiyo ushauri wetu, wakandarasi wakigeni wanaopata miradi hapa nchini lazima tuhakikishe wanabakisha ujuzi wao kwa wataalamu wetu wazalendo ili ilifikie pahala tuweze kusimama sisi wenyewe.

Tunaweza pia kuangalia kwa jicho la tatu sekta ya bahari kama inavyoitwa ‘blue economy’, kwa wakaribisha wawekezaji kwenye uvuvi wa bahari kuu sasambamba na kuwekeza viwanda cha kuchakata na kusindika samaki.