WASHINGTON, MAREKANI

RAIS mteule wa Marekani Joe Biden amewasili Washington katika mkesha wa sherehe ya kuapishwa kwake, wakati mtangulizi wake Donald Trump ambaye atasusia hafla hiyo ya kula kiapo kwa mara ya kwanza akiitakia mafanikio serikali mpya.

Machozi yalimtoka Biden katika sherehe ya kuagwa mjini Wilmington, Delaware, ambako alitoa heshima kwa marehemu mwanawe wa kiume kabla ya kupanda ndege kuelekea katika mji mkuu.

Kwa upande wake, Trump ambaye hajaonekana hadharani kwa wiki moja sasa, alivunja ukimya wake wa siku nyingi kupitia hotuba iliyorikodiwa kwenye mkanda wa video.

Trump kwa mara ya kwanza aliwaomba Wamarekani kuiombea mafanikio serikali ijayo ya Biden, ikiwa ni mabadiliko ya msimamo wa wiki nyingi alizotumia kuishawishi idadi kubwa ya wafuasi wake wa Republican kuwa Mdemocrat huyo alifanya udanganyifu katika kinyang’yiro cha urais.