JANUARI 20 mwaka huu tulishuhudia Joe Biden akiapishwa kama rais wa 46 wa Marekani, lakini rais huyo mpya ameweka historia kuwa mtu mwenye umri mkubwa katika hostoria ya nchi hiyo kuchukua madaraka ya urais.

Katika sherehe za kuapishwa na kubadilisha madaraka kwa ujumla, yapo mambo yalifanywa hadharani kama wengi wetu tulivyoona, lakini yapo mambo mengine makabidhiano yalifanyika kwa siri.

Moja wapo ya tukio linalofanyika kwa siri wakati wa viongozi kubadilishana madaraka nchini Marekani ni hatua ya rais anayemaliza muda wake kumkabidhi rais anayeingia madarakani sanduku la nyuklia.

Kwa takriban miongo sita sasa, wakati wa kuapishwa kwa rais mpya nchini Marekani, hafla inayofanywa nyuma ya pazia ni wanajeshi wawili waliovalia sare hukaa pembeni kwenye hafla ya kuapishwa rais mpya.

Mmoja wao, ambaye huandamana na rais anayeondoka madarakani katika safari zake nyingi, hubeba sanduku zito ambalo humkabidhi sanduku hilo ofisa mwingine ambaye atakuwa akiandamana na rais mpya.

Sanduku hili ndilo inaloitwa ‘black box’ ama sanduku la nyuklia. Sanduku hilo limetengenezwa kwa chuma huambatana na rais wa Marekani kila mahali anapokwenda iwapo anataka kurusha bomu la kinyuklia akiwa nje ya ofisi yake.

Tangu sanduku hilo lilipoanza kutumika wakati wa utawala wa rais John F Kennedy, ubebaji wa sanduku hilo umekuwa kitu muhimu licha ya kutokuwa miongoni mwa vitu muhimu katika sherehe hiyo ya kumuapisha rais mpya nchini Marekani.

Hata hivyo, mwaka huu njia rahisi ya kukabidhi sanduku hilo kutoka mkono mmoja hadi mwingine ilikabiliwa na changamoto kubwa kwa mara ya kwanza katika zaidi ya karne moja, hasa ikizingatiwa kuwa rais anayeondoka mamlakani hakuwepo katika halfa ya kumuapisha mrithi wake.

Kulingana na itifaki, Trump alipaswa kuwa na sanduku hilo la nyuklia hadi saa sita za mji wa Washington, lakini hadi kfikia wakati huo tayari alikuwa umbali wa kilomita 1,500 kutoka ikulu ya ‘white house’.

Trump alipaswa kkabidhi sanduku hilo, lakini wakati Biden anaapishwa Trump alikuwa katika mji wa Florida akikwepa kuhudhuria sherehe hizo za kubadilishana madaraka.

Hata hivyo kuna masunduku kama hayo kulingana na watalaamu ambayo huwa tayari kutumika katika matukio kama hayo, Hivyo basi tunauliza je hafla hiyo ya kukabidhiana sanduku hilo la kinyuklia inafanyika vipi iwapo marais hao walikuwa maeneo tofauti?

Katika hafla ya mwaka huu kuna wasiwasi kama sanduku hilo lilikabidhiwa kwa utawala wa Biden, hata hivyo Idara ya ulinzi nchini Marekani hivi majuzi ilieleza kwamba ilikuwa na mpango wa siku ya kuapishwa kwa rais mpya kukabidhi sanduku hilo, lakini ikakataa kutoa maelezo.

Hata hivyo, wataalam kadhaa na wasomi walielezea matukio kadhaa yanayoweza kufanyika iwapo hali hiyo isiyo ya kawaida itafikia hapo katika historia ya Marekani.

Wakati wa hafla ya mtaalamu wa kituo cha udhibiti wa silaha, Stephen Schwartz, alielezea kwamba tofauti na fikra za wengi, lakini kuna masunduku matatu ya aina hiyo.

Moja ni lile linaloandamana na rais, lakini kuna orodha nyingine ya dharura anayopewa makamu wa rais ama waziri ambaye huteuliwa kuchukua mamlaka iwapo kwa sababu fulani viongozi wote wamefariki.

Schwartz alisema kwamba Pentagon inaweza kutumia moja wapo ya masunduku yake ama kuandaa jipya ili kumkabidhi Biden na kulifanya kuweza kufanya kazi punde Biden atakapoapishwa.

Wakati huo, usimamizi wa Trump wa nyuklia na udhibiti umemalizika, hivyo basi kadi zake zinazotoa nambari hizo za siri za sanduku hilo la nyuklia huzimwa rasmi.

“Iwapo ofisa anayebeba sanduku hilo aliandama na Trump katika ndege ya Airforce One kuelekea Florida, msaidizi huyo ataondoka mahala alipo Trump mwendo wa saa sita kamili na kurudi Washington na sanduku hilo, Schwartz aliambia CNN.

Ni hali hiyo ambayo suala la sanduku hilo limezua maswali mengi na matumizi yake yamewavutia mamilioni ya watu miaka yote.

Hata hivyo kile ambacho watu hawakijui ni kwamba nambari za siri na funguo zake katika sanduku hilo ambazo zinamruhusu rais kuwa na uwezo wa kutoa maagizo ya kutekeleza shambulio hazipo katika sanduku hilo.

Funguo hizo za uwezo wa kutekeleza shambulio la kinyuklia huwa ni kadi ndogo ya plastiki ambayo rais aliye madarakani hubeba mfukoni. Kadi hiyo hujulikana kama ‘’Code of Gold au Cookie’.

Rais hutakiwa kuikata mara mbili ili kuthibitisha utambulisho wake anapowasiliana na kitengo cha vita katika Pentagon, ili kuruhusu shambulio.

Mapema siku ya kuapishwa kwa rais, rais mpya na makamu wake hupokea maagizo ya jinsi ya kutumia sanduku hilo na rais anayechukua mamlaka hupatiwa kadi hiyo.

Kulingana na jarida la sayansi ya atomiki, Pentagon huzima kadi ya rais anayeondoka madarakani saa sita siku ya kuapishwa kwa rais mpya huku kadi ya rais mpya ikiwashwa.

Hivyo basi saa sita na dakika moja Januari 20, kwa mfano iwapo Trump angetaka kutekeleza shambulio la kinyuklia, asingeweza kufanya hivyo, iwapo bado alikuwa anamiliki sanduku hilo na Biden naye asingeweza kufanya hivyo saa tano na dakika 59 asubuhi.

Hofu kwamba Trump angetekeleza shambulio la nyuklia kabla ya kuondoka kwake katika serikali ilizua wasiwasi kufuatia ghasia za uvamizi wa jengo la bunge la Capitol Hill mapema mwezi huu.

Wakati huo kiongozi wa bunge hilo Nancy Pelosi, aliwasiliana na idara ya ulinzi na kuwataka kutofuata maagizo ya Trump iwapo angetaka kutekeleza shambulio hilo kabla ya kuondoka katika ikulu.

Bruce Blair, mwanachama mstaafu wa kundi la timu ya kutekeleza shambulio la nyuklia nchini Marekani, alieleza kwamba tofauti na jinsi watu wanavyoamini, sanduku hilo la nyuklia halina kitufe ama nambari za siri zinazomwezesha rais kutekeleza shambulio la nyuklia moja kwa moja, na badala yake itifaki za shambulio hilo ni sharti awasiliane na washauri wa ngazi za juu.

“Katika sanduku hilo pia kuna mchoro wa mpango wa vita, malengo yake pamoja na idadi ya watakaofariki bila kusahau silaha zilizopo, hivyo basi ni rahisi kuelewa hali ilivyo katika sekunde chache”, alisema Blair.

Ndani ya sanduku hilo si nambari za siri pekee za kutekeleza shambuliko hilo la uharibifu, pia kuna vitabu viwili, ambapo kimoja kina maelezo ya kina kuhusu aina ya shambulio hilo la nyuklia ambalo linaweza kutekelezwa na orodha nyingine ya maeneo salama kwa rais wa Marekani na familia yake kujificha.

Wakati mwingi sanduku hilo huonekana na antena iliyojitokeza ambayo hutumika kuimarisha mawasiliano ya moja kwa moja na idara ya ulinzi The Pentagon.