WASHINGTON, MAREKANI

MARA baada ya kuapishwa kuwa rais wa 46 wa Marekani, Joe Biden amesaini amri 17 za utekelezaji ambazo zimetengua maamuzi yaliyopitishwa na mtangulizi wake Donald Trump.

Katika siku ya mwanzo baada ya kuingia Ikulu ya White House rais mpya wa Marekani alisaini amri 17 za utekelezaji kwa lengo la kubatilisha hatua kadhaa zilizochukuliwa na Trump.

Kuondoa marufuku ya kusafiri kuelekea Marekani raia wa nchi za Kiislamu, kuirejesha Marekani kwenye Makubaliano ya Paris ya tabianchi, kusimamisha mchakato wa kujitoa nchi hiyo katika Shirika la Afya Duniani WHO, kulazimisha watu wote kuvaa barakoa katika maeneo ya umma na kuhitimisha hali ya hatari katika mpaka wa pamoja wa Marekani na Mexico ni miongoni mwa amri za utekelezaji zilizosainiwa na Biden.

Wakati akisaini amri hizo, rais mpya wa Marekani alisema,ni matumaini yake kuwa amri alizosaini zitaleta mabadiliko katika janga la dunia nzima la Covid-19 na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kufuta amri na kusitisha sera zilizotekelezwa wakati wa urais wa Donald Trump ilikuwa moja ya ahadi kuu alizotoa Biden wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais.

Sherehe za kuapishwa Joe Biden kuwa rais mpya wa Marekani zilizofanyika Januari 20 zilikuwa na hali tofauti kuwahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hiyo.

Kwa kuhofia kutokea tena fujo zilizofanywa tarehe 6 Januari na wafuasi wa Trump za kuvamia jengo la Kongresi, hatua kali za usalama zilichukuliwa na kutawala anga ya hafla ya kuapishwa na kukabidhiwa madaraka Biden.

Aidha, kinyume na ilivyo ada na desturi, Donald Trump alikataa kuhudhuria hafla hiyo ya kuapishwa rais huyo wa 46 wa Marekani.