Na Ali Shaaban Juma

Usafirishaji wa bidhaa mbalimbali ulimwenguni ni moja ya harakati za kiuchumi zinazounganisha mataifa ya mabara tofauti. Usafirishaji wa bidhaa mbalimbali duniani huchangia asilimia 25% ya uzalishaji wa bidhaa ulimwenguni ambapo mafuta ndiyo bidhaa inayosafirishwa kwa wingi duniani kote.

Zaidi ya mataifa 50 duniani kote yanategemea mafuta kama bidhaa kuu inayosafirishwa nchi za nje na kuingiza fedha za kigeni kwa mataifa hayo.

Tokea mwaka 2000, usafirishaji wa bidhaa na huduma kutoka nchi moja hadi nyengine umeongezeka mara dufu ulimwenguni na kufikia thamani ya Dola Trilioni 19.5.

Katika makala haya tutaelezea baadhi ya bidhaa kuu zinazosafirishwa na kila nchi duniani ambapo bidhaa hiyo ndiyo inayosafirishwa kwa kiwango kikubwa kuliko bidhaa nyengineyo.

Kitu cha msingi kufahamu hapa ni kwamba viwango hivyo vya kusafirisha bidhaa hizo vinaweza kubadilika kutokana na mabadiliko ya mahitaji ya bidhaa katika soko la dunia na mabadiliko ya mtazamo wa kisiasa kati ya taifa moja na mataifa mengineyo.

Huko Marekani ya Kaskazini, eneo ambalo linajumuisha mataifa ya Marekani, Canada, Mexico na Greenland, Marekani na Canada zinasafirisha kwa wingi mafuta ya Petroli ambapo Mexico inasafirisha kwa wingi magari. Nayo Greenland nchi iliyoko kaskazini mwa dunia ni masafrishaji mkubwa wa samaki.

Greenland  kisiwa kidogo chenye uhuru wa ndani chenye wakaazi 57,000 kilioko ndani ya ardhi ya Denmark hapo mwaka jana kilisafirisha samaki, kamba na mazao mengine ya baharini yenye thamani ya Dola Bilioni 1 ikiwa ni wastani wa asilimia 80.9 ya mauzo ya nje ya nchi hiyo. Wengi wa samaki hao na mazao mengineyo ya baharini huuzwa nchini Denmark, Latvia, Ureno, Urusi, Iceland, Norway na Thailand.

Kutokana na udogo wa kisiwa hicho na idadi ndogo ya watu 57,000 wanaoishi katika kisiwa hicho kila mtu wa kisiwa hicho anapata wastani wa Dola 22,700 kwa mwaka.

Huko Marekani ya Kusini na visiwa vya Caribbean, nchi za visiwa zinazosafirisha nje Petroli ni pamoja na Trinidad na Tobago, Saint Vicente, Saint Lucia, Bonaire, Curacao na visiwa vya Turks and Caucus.

Kinachofurahisha ni kwamba kisiwa cha Haiti, Nicaragua, Honduras na El Salvador ni wasafirishaji wakubwa wa  fulania za T-Shirt ambapo kisiwa cha Montserrat ni msafirishaji mkubwa wa mchanga.

Visiwa vya Cayman Na British Virgin vinasafirisha boti za kifahari ambapo visiwa vya Antigua na Barbuda, Bahamas, Netherlands Antilles vinatengeneza na kusafirisha meli kubwa za kitalii.

Vifaa vya umeme vinasafirishwa na visiwa vya Saint Kitt na Nevis ambapo Jamaica inasafirisha madini ya Aluminium. Cuba ni msafirishaji mkubwa wa sigara aina ya Cigar ambapo mwaka 2019, taifa hilo lilisafirisha Cigar za Dola Milioni 5.

Nayo Jamhuri ya Dominica inasafirisha dhahabu. Visiwa vya Anguilla na Barbados ni wasafirishaji wa pombe ambapo kisiwa cha Saint Martin kinasafirisha vito vya thamani.

Dominica na Costa Rica ni wasafirishaji wa vifaa vya matibabu ambapo Grenada husafirisha kungu manga. Grenada ambayo ni nchi ya pili kwa kuzalisha Kungu manga kwa wingi duniani baada ya Indonesia, mwaka jana ilisafirisha Kungu Manga, Hiliki na maganda ya kungu manga (basibasi) zenye thamani ya Dola Milioni 9.

Nchi za Panama, Venezuela, Colombia, Equador, Bolivia na Colombia ni wasafirishaji wa petroli ambapo Peru na Chile ni wasafirishaji wa shaba.

Wakati visiwa vya Falkland ni masafirishaji mkubwa wa mazao ya baharini yakiwemo pweza, chaza, kamba na samaki, Belize ni msafirishaji wa miwa na sukari ambapo Guatemala ni msafirishaji wa ndizi. Katika mwaka 2018, Guatemala ilisafirisha ndizi zenye thamani ya Dola Bilioni 1.35 ambapo wanunuzi wakuu wa bidhaa hiyo walikuwa ni Marekani, Canada, China, Mexico na El Salvador.

Guyana na Suriname ni wasafirishaji wa dhababu ambapo Brazil na Paraguay ni wasafirishaji wa Maharagwe aina ya Soya. Katika mwaka 2018, Brazil ilisafirisha nje ya taifa hilo tani milioni 75 za maharagwe aina ya Soya yenye thamani ya Dola Bilioni 33.2 ambapo wanunuzi wakuu wa bidhaa hiyo walikuwa ni China na Hispania.

Argentina inasafirisha mafuta yatokanayo na mbegu mbali mbali na Uruguay inasafirisha mbao zinazotumika kutengeneza karatasi.

Barani Ulaya bidhaa inayosafirishwa kwa wingi na bara hilo ni gari ambapo mataifa 14 ya bara hilo yanauza nje gari kama bidhaa kuu inayosafirishwa nje ya bara hilo.

Katika mwaka 2019, Jumuiya ya Ulaya ilisafirisha gari Milioni 5.6  ambapo gari milioni 1,568,000 ambazo ni sawa asilimia 28 ya gari  hizo zilisafirishwa nchini Marekani. Gari 924,000 sawa na asilimia 16.5 zilisafirishwa nchini China.

Kwa upande wa usafirishaji wa bidhaa kwa nchi moja moja, Albania ni nchi inayosafirisha kwa wingi viatu barani ulaya ambapo asilimia 80 ya pato la taifa hilo linatokana na mauzo ya viatu.

Nchi za Ulaya ambazo bidhaa yake kuu inayosafirishwa nje ni mafuta ya petrol ni pamoja na Belarus, Bulgaria, Ugiriki, Gibraltar, Finland, Uholanzi, Norway, Urusi, Lithuania, Croatia na Cyprus. 

Nchi zinazosafirisha kwa wingi gari ndogo barani ulaya ni Jamhuri ya Czech, Ubelgiji, Slovakia, Slovenia, Sweden,  Ureno, Uingereza, Hispania na Austria.

Ukraine ni taifa pekee barani Ulaya ambalo bidhaa kubwa inayosafirishwa nje ya nchi hiyo ni mbegu za alizeti.

Romania inasafirisha kwa wingi magari makubwa ambapo barani ulaya nchi inayosafirisha ndege kwa wingi ni Ufaransa.

Ufaransa nchi ya sita yenye uchumi mkubwa duniani, hapo mwaka 2018, ilisafirisha ndege, Helikopta na vifaa vya anga za juu vyenye thamani ya Dola Bilioni 43.8. Wanunuzi wakuu wa ndege hizo za Ufaransa ni pamoja na Marekani, China, India, Ujerumani na Qatar.

Bidhaa zinazosafirishwa kwa wingi na Italia na Denmark ni dawa ambapo Italia ndiyo mzalishaji mkubwa wa dawa barani Ulaya. Zaidi ya wafanyakazi 66,000 wameajiriwa katika viwanda vya dawa nchini  humo ambapo taifa hilo  la Italia linauza asilimia 2.8 ya dawa zote zinazouzwa ulimwenguni.

Makampuni makubwa ya dawa ya Italia ni pamoja na Menarini, Chiesi na Angelini ambapo mwaka 2019 mauzo ya dawa ya Italia katika soko la dunia yalifikia Dola Bilioni 18.6.

Latvia ni msafirishaji mkubwa wa mbao barani  ulaya ambapo bidhaa kubwa inayosafirishwa na  Ireland ni damu. Damu inayosafirishwa na Ireland nje ya taifa hilo ni ile inayochangwa kutoka kwa watu mbalimbali nchini humo ambapo mwaka 2018, taifa hilo liliuza nje damu yenye thamani ya Dola Bilioni 7.10 ambapo damu hiyo iliuzwa nchini Marekani, Ubelgiji na Uingereza.

Serbia na Moldova zinasafirisha zaidi waya ambapo Andora na Estonia ni wasafirishaji wakubwa wa vifaa vya umeme.

Bidhaa kubwa inayosafirishwa na Uswiss ni dhahabu ambapo Montenegro inasafirisha kwa wingi Aluminium. Nayo nchi ndogo ya San Marino ni msafirishaji mkubwa wa aina mbalimbali za mashine.

Huko barani Asia, nchi zinazosafirisha kwa wingi Petroli ni pamoja na India, Saudia, Iran, Oman, Yemen, Kuwait, Bahrain, Iraq, Brunei, Myanmar, Kazakhstan, Azerbaijan, Turkmenistan,  Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Qatar.

Afghanistan ni taifa pekee barani Asia ambalo bidhaa kubwa inayosafirishwa nje na taifa hilo ni zabibu ambapo moja ya tano ya bidhaa zinazosafirishwa nje ya taifa hilo zinatokana na zabibu. Katika mwaka 2019, taifa hilo liliuza nje zabibu zenye thamani ya Dola 237 Milioni.

Wakati ambapo Syria ni msafirishaji mkuu wa mafuta ya zaituni, Jordan ni msafirishaji mkuu wa mbolea nayo Israel husafirisha kwa wingi Almasi.

Nchi za Asia zinazosafirisha kwa wingi dhahabu ni pamoja na Tajikistan, Uzbekistan na Kirgizstan na Hong Kong ambapo Bangladesh ni msafirishaji mkubwa wa suti.

Katika mwaka 2918, Bangladesh ilisafirisha suti zenye thamani ya Dola Bilioni 6.9. Wanunuzi wakuu wa suti za Bangladesh ni pamoja na Marekani, China, Uingereza, Japan, Ujerumani na Sweden.

Bidhaa kuu inayosafirishwa na Japan ni magari ambapo Korea ya Kaskazini na Macao ni wasafirishaji wakuu wa saa za mkononi.

Mataifa yanayosafirishwa kwa wingi vifaa vya umeme na eletroniki barani Asia ni pamoja na Singapore, Korea ya Kusini, Vietnam, Malaysia pamoja na Philippines. Thailand ni msafirishaji mkubwa wa aina mbalimbali za mashine.

Wakati China inaongoza kwa kusafirisha vifaa vya umeme, Pakistani ni msafirishaji mkubwa wa magodoro, Uturuki inasafirisha kwa wingi gari.  Armenia na Georgia ni wasafirishaji wakuu wa shaba ambapo Indonesia na Mongolia zinasafirisha kwa wingi Makaa ya mawe. Kutokana na sababu za kijografia Laos ndiyo nchi inayosafirisha kwa wingi umeme katika nchi mbalimbali jirani.

Sir Lanka taifa ambalo ni la nne kwa kuzalisha chai kwa wingi duniani ni msafirishaji mkuu wa  chai ulimwenguni.   Wanunuzi wakuu wa chai ya Sir Lanka ni pamoja na mataifa ya Ulaya, Mashariki ya Kati, Marekani, China na Japan.Visiwa vya Maldives na vile vya British Indian Ocean Territory ni wasafirishaji wakubwa wa samaki.

Bidhaa zinazosafirishwa kwa wingi nchi za nje kutoka barani Afrika ni pamoja na Petroli, Makaa ya Mawe, Dhahabu, Almasi na Gesi Asilia. Msafirishaji mkuu wa kahawa barani Afrika ni Ethiopia ambapo hapo mwaka 2018, taifa hilo lilisafirisha kahawa yenye thamani ya dola Bilioni 1.

Zaidi ya mataifa 60 duniani yananunua kahawa kutoka Ethiopia zikiwemo Ujerumani, Saudia, Marekani, Italia, Sweden, Urusi, Jordan, Taiwan, Ugiriki na China.

Madagascar kwa upande wake ni mzalishaji na masafirishaji mkuu wa Vanila barani Afrika. Morocco ni taifa pekee barani Afrika linalosafirisha nje gari kama bidhaa kubwa inayosafirishwa na taifa hilo. Wakati Tunisia inasafirisha waya kwa wingi, nchi za Algeria, Libya, Misri, Sudan Kusini, Chad, Cameroon, Angola, Nigeria na Togo zinasafirisha kwa wingi Petroli.

Nchi zinazosafirisha kwa wingi dhahabu barani Afrika ni pamoja na Tanzania, Uganda, Afrika ya Kusini, Zimbabwe, Burundi, Rwanda, Mali, Bukina Faso, Ghana, Niger, Guinea, Liberia na Senegal. Senegal na Sao Tome zinasafirisha kwa wingi Cocoa ambapo bidhaa inayosafirishwa kwa wingi na Gambia na Guinea Bissau ni njugu. Kenya ni msafirishaji mkubwa wa chai ambapo Somalia na Djibouti ni wasafirishaji wakubwa wa Mbuzi na Kondoo.   Visiwa vya Seychelles, Mauritius na Cape Verde vinasafirisha kwa wingi samaki ambapo bidhaa kuu inayosafirishwa nje na Comoro ni karafuu.

Madini ya Zinc yanasafirishwa kwa wingi na Eritrea ambapo Msumbuji ni msafirishaji mkubwa wa Makaa ya Mawe. Nayo Benin ni msafirishaji mkubwa  wa pamba.

Sierra Leone ni taifa pekee barani Afrika linalochimba na kusafirisha kwa wingi madini yaitwayo Titanium ambapo wasafirishaji wakubwa wa shaba barani humo ni Congo DRC na Zambia ambapo Mauritania ni msafirishaji mkubwa wa chuma.

Wakati Malawi inasafirisha tumbaku, Jamhuri ya Afrika ya Kati ni msafirishaji mkubwa wa mbao.

Katika eneo la Oceania linalojumuisha Australia, New Zealand na visiwa kadhaa vilivyo katika bahari kuu ya Pasifiki kuzunguka eneo hilo, visiwa ya Mariana na Guan vinaafirisha chuma chakavu ambapo visiwa vya Marshall, Cooks, Niue na Tokelau vinasafirisha boti za kifahari na meli.

Visiwa vya eneo hilo la Oceania vinavyosafirisha samaki ni pamoja na Tonga, Fiji, Samoa, Tuvalu, Kiribati, Micronesia na Palau.

Visiwa vya Nauru na Chrismas vinasafirisha Chokaa ambapo visiwa vya Futuna na Wallis vinasafirisha vipuri vya magari. Petroli husafirisha na visiwa vya American Samoa na Timor Leste. Papua New Guinea husafirisha dhababu ambapo visiwa vya Cocos husafirisha aina mbalimbali za mashine. Australia ni mafirishaji wa makaa ya mawe ambapo New Zealand husafirisha maziwa.

Hata hivyo kwa uapnde wa usafirishaji wa bidhaa za jumla, nchi zinazosafirisha chakula kwa wingi duniani ni Marekani, Ujerumani, Uingereza na China.  Kwa uapnde mwengine, nchi zinazosafirisha nguo kwa wingi duniani ni  China, Jumuiya ya Ulaya, Marekani, India na Uturuki.

Kinachofurahisha zaidi ni kwamba nchi zinazosafirisha ubani wa kuchakua kwa wingi duniani ni Mexico ikifuatiwa na China, Canada, Uturuki na Uholanzi. Nazo nchi zinazosafirisha kwa wingi karatasi za kutumia chooni (toilet paper) ni China ikifuatiwa na Ujerumani, Italia na Sweden. Nazo nchi zinazosafirisha kwa wingi kinywaji cha Bia duniani ni Mexico ikifuatiwa na Uholanzi, Ubelgiji na Ujerumani.