Yasema inachangia migogoro Pemba
NA MWAJUMA JUMA
BODI ya ligi kuu Zanzibar imesema mgogoro uliopo katika kamati tendaji ya Shirikisho la soka Zanzibar (ZFF) umekuwa ukiathiri utendaji wa kazi zao.
Hayo yameelezwa na mjumbe wa bodi hiyo Mohammed Masoud alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko ofisi za ZFF Amaan.
Alisema licha ya bodi hiyo kufanya kazi vizuri lakini inaonekana inaongoza ligi upande wa Unguja peke yake, jambo ambalo sio sahihi kulingana na kanuni na katiba ya ZFF
“Kuna msuguano ambao unasababishwa na kamati tendaji sisi bodi hatutakiwi kuingilia, lakini tulitakiwa kujua kwa sababu sisi ndio wenye dhamana ya mpira, wengine wana dhamana ya uongozi, hivyo sisi wenye dhamana ya mpira katika kipindi hiki tumefikia dirisha dogo lakini upande mmoja hakuna ligi iliyoendelea”, alisema.
Alieleza kila mmoja ni shahidi wa hayo, kwamba ligi katika kisiwa cha Unguja inaendelea lakini Pemba hata usajili haujafanyika.
Hivyo waliitaka kamati tendaji kuwajibika kwa nini ligi inachezwa upande mmoja, wakati kanuni ya mashindano na ratiba zote ni moja na hakuna ligi mbili katika nchi moja.
“Kulikuwa na timu nyingi sana, tukafanya mikutano ya mara kwa mara, hadi tukafikia Zanzibar kuwa na ligi moja ya timu 12 za ligi kuu, na kanda kwa kila upande, hatimae tukatoa timu mbili kupanda moja kutoka kila upande, suala ambalo sasa halifanyiki na inaelekea mgogoro huo utaendelea kuwepo hadi mwaka 2025”, alisema.