KINSHASA,DRC
RAIS Faustin-Archange Touadera ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 27 Desemba katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Matokeo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo yalimpa Touadera asilimia 53 ya kura zilizopigwa.
Mwenyekiti wa tume hiyo Mathias Morouba alisema kwa ushindi huo wa kishindo, anamtangaza Touadera kuwa mshindi wa uchaguzi huo.
Morouba alisema watu wapatao 910,000 ambao ni nusu ya wote wenye sifa za kupiga kura nchini humo walijiandikisha, na kati yao asilimia 76.3 walishiriki katika zoezi la uchaguzi.
Uchaguzi huo uligubikwa na mashambulizi ya waasi watiifu kwa rais wa zamani Francois Bozize, walioazimia kuuvuruga.
Duru za hivi punde zinaarifu kuwa waasi hao waliukamata mji muhimu wa Bangassou ulio kusini mashariki, na kuwalazimisha wakaazi wake kukimbilia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.