NA LAYLAT KHALFAN

MWAKILISHI wa jimbo la Tumbatu, Haji Omar Kheri, amesema watahakikisha wanaitekeleza vyema ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM kwa vitendo pamoja na kukamilisha ahadi walizokubaliana na wananchi wakati wa kampeni.

Mwakilishi huyo, aliyasema hayo Tumbatu wakati wakitoa shukran zao kwa wananchi wa shehia mbili Gomani ‘A’ na ‘B’ kwa kuwachagua kwa kishindo kikubwa kwa kupata kura nyingi za ndio.

Alisema ahadi ya chama ni kutekeleza ilani hiyo ndani ya miaka mitano haijaalishi kwamba wataanza mwanzo wa mwaka au mwishoni, lakini kinachotakiwa ni kukamilisha ahadi hizo mapema, ili wananchi waweze kunufaika.

Alisema kupitia ilani hiyo kuna mambo kadhaa ambayo yanahitaji kufikishiwa wananchi ikiwemo afya, skuli, maji, umeme, barabara, miradi mbalimbali ikiwemo vikundi vya ushirika kwa lengo la kuwaondoshea wananchi hali ngumu ya kimaisha.

Alisema kutokana na kuwa huduma hizo bado wananchi hazijawafikia ipasavyo, atahakikisha anaziimarisha kwa wakati ili lengo lililokusudiwa liweze kufikiwa.

Akigusia kuhusu vikoba, alisema vikoba vingi vinakufa licha ya kupatiwa fedha nyingi za kujiendeshea, wengi wao wanajisahau na kuzitumia vibaya isivyostahiki.

“Mara hii sitoi pesa za vikoba kama hatujatoa elimu kwanza ya ujasiriamali naona sielewi pesa zinatumika vibaya sana na kinachofanywa hatukioni”, alisema.

Akizungumzia kuhusu uvuvi haramu, Mwakilishi huyo alisema suala hilo limeshamiri na kurudisha nyuma uchumi wa buluu hivyo atatumia kila jitihada kuona ndani ya jimbo hilo hali hiyo haiendelei.

Alisema wamegundua kuwa hivi sasa wanyama wengi adimu kama vile chwale, pomi, vichomi, mwata, kaa bamba na wengine kadhaa wamepotea baharini kutokana na wavuvi kushindwa kuzingatia matumizi mazuri ya bahari.

Aidha, aliwataka masheha na viongozi wa jimbo hilo kushirikiana kwa pamoja katika kuunga mkono jitihada zinazopelekwa na viongozi ili waweze kusonga mbele kimaendeleo.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo, Juma Othman Hija, alishauri wananchi jimboni humo wasijibweteke na ushindi mkubwa walioupata na badala yake wakaze buti ili waweze kujenga taifa lao.

Nao wananchi wa shihia hizo mbili walisema wamefurahishwa na uamuzi uliochukuliwa na viongozi wao kwa kwenda kurudisha shukran,hivyo waliahidi kuwa nao bega kwa bega katika kipindi chote cha uongozi wao kwa kuona malengo waliyokusudia kuyatekeleza jimboni humo yanafikiwa.