FELIX Tshilombo Tshisekedi rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambaye tangu achukue madaraka anaonekana kama amependia punda, lakini hatamu za kumuongoza punda huyo ziko mikononi mwa mtu mwengine.

Sehemu kubwa ya madarakana serikali na hata katika bunge la DRC, wanasiasa wa rais wa zamani Joseph Kabila ndio waliotawala sehemu kubwa ya maamuzi ya kisheria na kisera.

Kwa hakika rais Felix Tshisekedi amejikuta kwenye wakati mgumu kwani pale anapotaka kumuongoza punda kwenye anayoitaka yeye kwa bahati mbaya sana mikononi anajikuta hana hatamu, hivyo mwenye hatamu ndiye anayemuongoza punda njia anayoitaka yeye.

Hata hivyo, mnamo mwanzoni mwa mwezi Disemba mwaka 2020, Tshisekedi alijaribu kufanya kila njia kuhakikisha hatamu zinaingia mikononi mwake ili aweze kumuongoza vyema punda aliyekabidhiwa na wananchi wa DRC.

Tshisekedi, aliamua kuuvunja ushirikiano wa kisiasa na muungano wa chama cha rais wa zamani Joseph Kabila Kabange, ushirika ambao uliundwa ili kumuwezesha Tshisekedi kuunda serikali kwa sababu ya kutopata wingi wa wajumbe bungeni kufuatia uchaguzi 2018.

Baada ya kulivua koti la muungano, hivi sasa kiongozi huyo anakabiliwa na kitandawili cha kuunda serikali kutokana na muungano mpya au alivunje bunge na kuitisha uchaguzi mwingine.

Mnamo Disemba mwaka 2018, Tshisekedi wa chama cha upinzani Union for Democracy and Social Progress (UPDS), aliingia madarakani katika mabadiliko ya kihistoria nchini DRC, baada ya kumshinda katika uchaguzi Emmanuel Ramazani Shadary.

Mgombea mwengine wa upinzani Martin Fayulu na chama chake LAMUKA walidai kuwa ndio walioshinda kwenye uchaguzi huo, hata hivyo tume ya uchaguzi nchini humo ikamtangaza Tshisekedi.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida katika siasa za Afrika, wafuasi wa Kabila kutoka muungano uliopewa jina la Common Front for Congo (FCC) walishinda karibu asilimia 70 ya viti bungeni, jumla ya wabunge 350.

UDPS asilimia 36 na mshirika wake Union for the Congolese Nation (UNC) chama cha Vital Kahmere asilimia 17. Kwa pamoja viti 46 pekee. FCC inalidhibiti pia Baraza la Seneti ambapo Kabila ni mjumbe wa kudumu.

Katika uchaguzi huo, Tshisekedi na kiongozi wa Union for the Congolese Nation (UNC) Vital Kamerhe, walikubaliana kushirikiana katika uchaguzi wa Rais na kumuachia Tshisekedi kuwa mgombea wao wa pamoja.

Ushirikiano wa Tshisekedi na Kamerhe, uliwashtuwa wanasiasa wenzao waliokuwa pamoja katika kambi ya upinzani, Jean Pierre Bemba kiongozi wa Movement for the Liberation of Congo (MLC) na Gavana wa zamani wa Katanga Moise Katumbi.

Walipokutana mjini Geneva Uswisi, wote waliafikiana kumuunga mkono Fayulu kuwa mgombea wa upinzani, lakini ghafla Tshisekedi na Kamerhe walitangaza kujitoa.

Ni miaka miwili tangu Tshisekedi alipoapishwa Januari 2019 na kuanza kuzikabili changamoto kubwa, wafuasi wa Kabila walisisitiza wapewe wizara kadhaa muhimu na walifanikiwa kwa sababu Tshisekedi hakuwa na chaguo jingine.

Aidha Kabila aliendelea kutaka kuwa na ushawishi kwenye uteuzi wa nafasi mbalimbali zikiwemo za uongozi jeshini. Akihisi amefungwa mikono, Tshisekedi sasa ameshindwa kuvumilia zaidi.

Hivi sasa Tshisekedi maarufu kwa wafuasi wake kwa jina la “Fatchi”, ameamua kukabiliana na Kabila, ambapo wiki chache zilizopita alitangaza kuvunja ushirikiano, lengo likiwa ni kuunda umoja mpya utakaokuwa na wingi bungeni ili taifa hilo liweze kusonga mbele. Ameupa jina “Umoja Mtakatifu”.

Tayari alionya ikiwa atashindwa, atalazimika kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi mpya. Katika hotuba yake mbele ya mabaraza yote mawili ya bunge Disemba 14 alisema,”Nimeivumilia hali hii, lakini uvumilivu huo haukutosha kuniwezesha kuongoza kwa utulivu”.

Awali wabunge 281 kati ya 500 walipiga kura kumuondoa Spika wa bunge Jeanine Mabunda. Wapinzani wa Kabila wamesherehekea kuondolewa Mabunda, rafiki yake wa chanda na pete. Amedaiwa kuendesha shughuli za bunge kwa ukereketwa.

Maofisa wa Tshisekedi wamekuwa mbioni kuwashawishi wanasiasa wa upinzani na wabunge wa FCC kujiunga na muungano mpya na kuna ishara kwamba mkakati umeanza kuzaa matunda.

Magavana wa mikoa 29 walitangaza kumuunga mkono Tshisekedi na ikidaiwa kuna kiasi cha wabunge 70 kutoka kambi ya Kabila na wanasiasa kadhaa ambao tayari wameashiria kuiacha mkono FCC akiwemo waziri wa zamani wa mawasiliano wa Kabila, Lambert Mende.

Tshisekedi pia aliwakaribisha kwa mazungumzo Bemba na Katumbi , mahasimu wengine wakubwa wa Kabila. Juhudi zake zinaonekana kuanza kuzaa matunda.

Akiukaribisha mwaka mpya 2021 Tshisekedi alichukua hatua isiyotarajiwa, alipotoa msahama kwa watu 23 waliokuwa gerezani, baada ya kuhukumiwa kuhusika katika mauaji ya Rais Laurent Desire Kabila 2001.

Miongoni mwao ni aliyekuwa mpambe na mlinzi wa kiongozi huyo Kanali Eddy Kapend na mkuu wa usalama wakati huo Georges Leta.

Wote walihukumiwa na mahakama ya kijeshi ambayo baadaye ilivunjwa. Kuachiwa huru watu hao wawili baada ya kuweko gerezani karibu miaka 20 pamoja wenzao 21 kumepokelewa kwa maoni tafauti. Wengi wamempongeza Tshisekedi, wakiamini wafungwa hao walikuwa ni muhanga wa mchezo wa kisiasa.

Kapend alisisitiza wakati wote kuwa hana hatia na kusema, ” Waliohusika na njama hiyo wanajijua na wako nje.” Wadadisi wanaamini Tshisekedi amejiongezea turufu kujitenga zaidi na Kabila, ingawa binafsi alisema msamaha huo ni zingatio la kiutu.

Uchaguzi ujao ni 2023, lakini haijafahamika ikiwa Tshisekedi atagombea muhula wa pili, lakini haijafahamika msimamo wa UNC utakuwaje ikiwa kiongozi wao Kamerhe ataendelea kubakia gerezani.

Juni 2020, Kamerhe aliyedhaniwa angekuwa waziri mkuu na badala yake akateuliwa Mkurugenzi wa ofisi ya Rais akiwa na jukumu la kusimamia shughuli za utawala Ikulu, alipatikana na hatia ya ubadhirifu wa mali ya umma na ufisadi.

Alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na kupigwa marufuku kushika wadhifa wowote wa serikali au utumishi wa umma kwa muda wa miaka 10.

Walipoafikiana kushirikiana, wanasiasa hao wawili walikubaliana kupokezana madaraka, Tshisekedi awe mgombea urais mhula wa kwanza na Kamerhe 2023, hata hivyo hukumu hiyo ikawa mwisho wa Kamerhe kisiasa.

Inaelekea Kabila ana kiu ya kubakia madarakani ambapo mnamo mwishoni mwa mwezi Disemba Kabila aliwasili Lubumbashi mji mkuu wa jimbo la Katanga na kulahikiwa na umati mkubwa wa wafuasi wake.

Wadadisi wanachokiona kuwa ni kupima joto la kisiasa likoje, ikizingatiwa mpinzani wake mkubwa jimboni humo ni Moise Katumbi aliyezuiliwa na Kabila kuwa mgombea 2018.

Miaka 60 ya uhuru kutoka kwa Ubeligiji 1960, Congo imepitia vipindi tafauti vya misukosuko ya kisiasa, kiuchumi na vita. Rais wa zamani Sese Seko aliyetawala kwa miaka 32 hadi alipoangushwa Mei 1997 alikuwa na msemo ” l état cést moi” (dola ni mimi).

Baada ya kuongoza kwa miaka 18, pengine Kabila naye anahisi Congo ni yeye. Wapambe wake wameanza kuzungumzia uwezekano wa kurudi na kugombea uchaguzi ujao 2023, wakisema hakuna cha kumzuwia.

Wakati ushirika wa Kabila na Tshisekedi sasa haupo tena, Wakongomani wanamkodolea macho Tshisekedi wakitumai atafanikiwa kuunda muungano mpya ili kama alivyoahidi, aanze safari yake ya kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi wanayoyasubiri kwa muda mrefu.

Ilimchukua muda wa miezi minane kuunda serikali ya mseto na FCC ya Kabila. Swali ni je itamchukua muda gani kuweza kupata uungaji mkono mpya na kuunda serikali imara, au kama alivyoonya atalazimika kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi mwengine?