LONDON, England

CHELSEA wamemfuta kazi meneja Frank Lampard baada ya kuiongoza kwa miezi 18, huku bosi wa zamani wa Paris St-Germain Thomas Tuchel akitarajiwa kuchukua nafasi yake.

Lampard, mwenye umri wa miaka 42, anaondoka klabuni hapo baada ya kichapo cha wiki iliyopita huko Leicester City, akiwa ameshinda mara moja katika mechi tano za ligi zilizopita.

Mchezo wake wa mwisho ulikuwa ushindi wa raundi ya nne ya Kombe la FA Jumapili dhidi ya Luton.

Lampard aliteuliwa kwa mkataba wa miaka mitatu wakati akichukua nafasi ya Maurizio Sarri huko Stamford Bridge mnamo Julai 2019.

Kiungo huyo wa zamani wa Chelsea aliwaongoza hadi nafasi ya nne na fainali ya Kombe la FA katika msimu wake wa kwanza wa uongozi, na ushindi wa 3-1 dhidi ya Leeds mwanzoni mwa Disemba uliiweka klabu hiyo kileleni mwa ligi kuu.

Katika taarifa yake, Chelsea ilisema: “Huu umekuwa uamuzi mgumu sana, na sio uamuzi ambao mmiliki na bodi wameuchukulia kidogo.

“Tunamshukuru Frank kwa kile alichofanikiwa wakati wake kama kocha mkuu wa klabu.Lakini matokeo na michezo ya hivi karibuni hayajafikia matarajio ya klabu.

“Hatuwezi kuwa na wakati mzuri wa kuachana na gwiji wa klabu kama vile Frank, lakini baada ya kufikiria kwa muda mrefu na kuzingatia iliamuliwa mabadiliko yanahitajika sasa ili kuipatia klabu muda wa kuimarisha timu na kupata matokeo mazuri msimu huu.”

Mmiliki Roman Abramovich alisema ‘’ulikuwa uamuzi mgumu sana kwa klabu, haswa kwa sababu nina uhusiano mzuri wa kibinafsi na Frank na ninamheshimu sana,” alisema Abramovich.

“Ni mtu wa uadilifu mkubwa na ana maadili ya juu zaidi ya kazi. Lakini  kwa hali ya sasa tunaamini ni bora kubadilisha mameneja.”