NA MWANDISHI WETU

CHINA imeahidi kuendeleza uhusiano wake na Zanzibar katika sekta mbali mbali zikiwemo za uchumi, utamaduni na ustawi wa jamii ikiwa ni muendelezo wa uhusiano uliodumu kwa muda mrefu sasa.

Balozi mdogo wa China, Zhang Zhisheng akitoa salamu za mwaka mpya ofisini kwake Mazizini, nje kidogo ya jiji la Zanzibar alisema China inathamini mchango wa Zanzibar katika jitihada zake za kupambana na ujinga, umasikini na maradhi ambazo zinapaswa kuungwa mkono na mataifa rafiki ikiwemo China.

Alisema juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha ustawi wa wananchi wa Zanzibar zimekuwa kivutio kikubwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na mara nyingi China imekuwa ikisaidia juhudi za mafanikio hayo.

“China imekuwa ikiitambua sana Zanzibar na itaendelea kufanya hivyo kutokana na uhusiano wa muda mrefu baina yetu ambao umeonekana kuwa na tija zaidi katika kufanikisha ustawi wa wananchi,” alisema na kuongeza kuwa uhusiano kati ya China na Zanzibar unapaswa kuimarishwa zaidi.

Balozi Zhang alisema licha ya kuwa China ni miongoni mwa nchi za mwanzo kuyatambua Mapinduzi ya Zanzibar imeendeleza uhusiano wake kwa kuchangia kuimarisha sekta za afya na ustawi wa jamii tokea mwaka 1964.

“Madaktari kutoka China walifika Zanzibar kwa mara ya kwanza mwaka 1964 lakini hadi sasa China imekuwa katika ramani ya Zanzibar katika uimarishaji wa sekta ya afya na itaendelea kwa lengo la kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi wa Zanzibar”, alisisitiza.

Akithibitisha hilo alisema China imesimamia ujenzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee, Pemba pamoja na kutoa michango mbali mbali ikiwemo ya vifaa vya tiba katika mapambano dhidi ya mripuko wa Covid-19 pamoja na magonjwa mengine yanayowasumbua wananchi nchini.

Kuhusu uimarishaji wa sekta za ustawi wa jamii, alisema China imechangia miundombinu katika sekta mbali mbali ikiwemo mawasiliano, michezo pamoja na udhamini wa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi nchini humo.

“Ukiondoa kipindi cha mripuko wa Covid-19, China imekuwa ikiongoza kwa kutoa ufadhili wa masomo ya muda mfupi na muda mrefu hasa kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Zanzibar, mpango ambao sasa umepungua kidogo” alisema na kuongeza kuwa udhamini wa mafunzo hayo utaendelea mara tu baada ya udhibiti wa Covid-19.

Balozi Zhang ambaye   anachukua nafasi ya Balozi Xie aliyemaliza muda wake hivi karibuni alithibitisha kuwa katika kipindi chote atakachokuwa Zanzibar atahakikisha uhusiano kati ya China, Zanzibar na Tanzania unaimarika.