NA MARYAM HASSAN
KAMISHANA wa Chuo cha Mafunzo, Ali Abdalla Ali amechukizwa na kitendo kinachofanywa na baadhi ya mahabusu ambao walipewa dhamana katika kipindi cha Corona kukimbia mahakamani.
Alisema fursa waliyopewa mahabusu na serikali ilikuwa na lengo la kupunguza mrundikano wa mahabusu hao ili kuwakinga na maradhi ya Corona.
Lakini alisikitishwa zaidi kuona kuwa mara baada ya kumaliza kwa kipindi hicho cha mpito mahabusu wengi wamekuwa wakikimbia mahakamani kwa ajili ya kuendelea na kesi zao.
“Kukimbia mahakamani sio suluhisho kwa sababu kesi zao zitakuwa zinasomwa kila tarehe iliyopangwa na hatimae kutolewa uamuzi kwa mujibu wa sheria na kama itabainika mmoja wao kuingia katika hatia popote alipo atakamatwa na kurudishwa katika gereza ili kutumikia adhabu yake” alisema Kamishna huyo.
Alisema licha ya kuwa Chuo cha Mafunzo, hawana jukumu la kufatilia mahabusu hao na wenye jukumu ni jeshi la polisi lakini katika kazi zao wamejenga mashirikiano makubwa baina yao.
Alisema kipindi cha Corona Serikali ilikaa pamoja na Mwanasheria Mkuu pamoja na Jaji mkuu ili kuona namna ambavyo itapunguza mrundikano wa mahabusu hao waliomo gerezani.
Alisema kupitia Jaji mkuu jumla ya dhamana 95 ilitolewa katika mahakama mbali mbali lakini kati yao baadhi yao ndio wanaofika mahakamani kwa ajili ya kuendelea na kesi zao.
Kwa upande wa Hakimu wa mahakama ya mkoa Mwera Said Hemed Khalfan, alisema watuhumiwa wengi wamekuwa wakizikimbia kesi zao mara baada ya kupewa dhamana.
Alisema suala hilo linaleta wakati mgumu katika mahakama hiyo kwa sababu kesi nyingi zinaondolewa kwa kukosekana washitakiwa pamoja na mashahidi.
“Tunaona kuwa wenzetu wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka wanachukua jitihada ya kutafuta mashahidi lakini shahidi akifika mshitakiwa hayupo au hata mda mwengine mshitakiwa anafika lakini shahidi hayupo” alisema
Aliiomba jamii kutoa ushirikiano huku akiwaasa wale ambao wanawachukulia dhamana washitakiwa wao wahakikishe kuwa wanatoa taarifa za watu wao mapema kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema ikiwa mdhamini wa mshitakiwa anashindwa kuwasilisha taarifa za mtuhumiwa wake mahakama haitosita kumchukulia hatua mdhamini huyo.