LONDON,UINGEREZA
MAOFISA wa Serikali ya Uingereza wametoa takwimu mpya zinazoonyesha kuwa zaidi ya watu elfu moja wamefariki kutokana na virusi vya corona katika siku 28 za hivi karibuuni.
Takwimu za Wizara ya Afya ya Uingereza zinasema kuwa, watu 1041 walifariki katika siku 28 zilizopita nchini humo kutokana na virusi vya corona.
Idadi hiyo inatambuliwa kuwa ni rekodi mpya tangu mwezi Aprili mwaka jana na inaonyesha kuongezeka tena maambukizi ya virusi vya corona nchini Uingereza.
Uingereza inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wahanga na waathirika wa corona barani Ulaya.
Nchi hiyo pia iliweka sheria kali za kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo ikiwa ni pamoja na kuwalazimisha wananchi kubakia majumbani mwao isipokuwa kwa kazi za dharura.
Wakati huo huo Marekani iliweka rekodi mpya kwa idadi ya watu wanaofariki dunia kutokana corona au COVID-19 kwa siku ambapo Jumanne iliyopita watu 3,936 walipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha John Hopkins, katika kipindi cha wiki moja iliyopita, kwa wastani watu 2,637 wamekuwa wakifariki dunia kila siku kutokana na corona nchini Marekani.Kwa msingi huo, kila sekunde 33 mtu moja amekuwa akifariki dunia nchini Marekani kutokana na corona.