MWAKA mpya unapoingia husherekewa kwa mbwembwe na staili tofauti katika nchi mbalimbali hapa dunianim wapo wanaopiga fataki, wapo wanaochoma matairi, wengine hula na kunywa na kadhalika.

Hata hivyo, wakati tunauaga mwaka 2020 na kuukaribisha mwaka 2021, nchini nyingi duniani zimesherekea mwaka mpya huku wananchi wakiwa kwenye kizuizi kikubwa kutokana na janga la ugonjwa wa corona.

Nchi nyingi duniani hasa barani Ulaya wananchi wanakabiliwa na vizuizi ili kudhiti ugonjwa wa corona, ambapo katika baadhi ya nchi kumeibuka aina mpya ya virusi vya corona.

Katika baadhi ya nchi ambazo zinakabiliwa na kasi kubwa ya maambukizi, zimepiga marufuku kabisa mikusanyiko ya kuuaga na kuukaribish mwaka mpya huku pia wananchi wakikatazwa kupiga fataki.

Miongoni mwa miji iliyopiga marufuku mikusanyiko na upigaji fataki ni pamoja na mji wa Sydney uliopo Australia na New York ulioko nchini Marekani, ambapo sherehe pia zimezimwa katika nchi za Ulaya.

Ufaransa iliweka zaidi ya polisi 100,000 kwa ajili ya doria katika barabara za mji mkuu mkesha wa mwaka mpya ili kuhakikisha amri ya kutotoka nje nyakati za usiku inazingatiwa.

Zaidi ya watu milioni 1.8 wamefariki kutokana na ugonjwa wa corona tangu janga hilo lilipoanza mwaka mmoja uliopita, huku takwimu zikibainisha kuwa watu wapatao milioni 81 wameripotiwa kuambukizwa virusi vya ugonjwa huo.

Nchini Ufaransa, serikali iliamuru uwepo wa usalama katika maeneo ya mijini kuanzia majira ya 2 nne usiku wa Alhamisi, wakati amri ya kutotoka nje ilipoanza, ambapo katika mji wa Paris nusu ya usafiri wa treni ulifungwa.

Ufaransa iliweka amri ya kutotoka nje huku mabaa, mikahawa na maeneo ya vivutio vya watu yakisalia kufungwa walipokaribisha mwaka mpya

Katika hotuba yake ya mwaka mpya, rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron aliwaeleza wakosoaji wanaolalamikia kujikokota kwa mpango wa kutoa chanjo, na kuapa kushughulikia suala hilo katika muda unaostahili.

Nchini Uingereza ambako virusi vipya vya corona vinavyosambaa kwa kasi vimegunduliwa huku watu milioni 20 wakiathiriwa zaidi katika eneo hilo watu wamelazimika kubakia majumbani mwao, ambapo waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson ametoa wito wa watu kuzingatia masharti yaliyowekwa.

Barabara za mji wa London zilikuwa kimya mkesha wa mwaka mpya baada ya polisi kuwataka wananchi washerehekee majumbani mwao.

Badala ya sherehe za kawaida zinazojumuisha mikusanyiko ya watu jijini London, onyesho la fataki lilifanywa katika maeneo tofauti jijini humo.

Ireland iliongeza vikwazo zaidi siku ya Disemba 31, kwa kupiga marufuku watu kutembeleana majumbani na kufunga maduka ambayo hayauzi bidhaa muhimu na kudhibiti usafiri wa hadi kilomita tano.

Ujerumani nayo imeweka amri ya kutotoka nje hadi Januari 10 mwaka huu. Serikali imepiga marufuku uuzaji wa fataki na kuweka vikwazo vikali vya kudhibiti idadi ya watu wanaokusanyika pamoja.

Katika hotuba yake ya mwaka mpya inayotazamiwa kuwa ya mwisho kwake kama kansela wa Ujerumani, Angela Merkel aliwaangazia watu wanaopotosha umma kuhusiana na janga hilo.

Alisema anashangazwa na jinsi uongo wa kijinga na wa kikatili unavyotumiwa bila kujali hisia za wale waliyopoteza wapendwa wao kutokana na ugonjwa wa corona.

Nchini Italia, amri ya kutotoka nje iliwekwa saa 4 usiku huku baa, mikahawa na maduka mengi yakifungwa, ambapo Papa Francis hakuongoza ibada ya mwaka mpya mjini Rome badala ya kupata maumivu ya nyonga sugu.

Uholanzi pia iko nchini ya amri ya kutotoka nje ambayo itaendelea kudumishwa hadi Januari 19 mwaka huu, ambapo hatua kama hizo pia zimechukuliwa nchini Uturuki.

Maofisa wameweka vikwazo vya kudhibiti sherehe za mwaka mpya katika majimbo mengi na miji ya nchi hiyo.

Mjini New York, mpira wa mraba wa taa uliwashwa wakati wa kuvuka mwaka, lakini eneo hilo halitakuwa wazi kwa umma.

Kikundi kidogo cha wafanyakazi wa kutoa huduma za afya ambao wanajulikana kama”shujaa wa 2020”. Na familia zao wataruhusiwa kuingia kama wageni maalum katika maeneo yaliyotengwa

Fataki zilipigwa marufuku katika miji tofauti nchini Marekani ikiwemo miji ya San Francisco na Las Vegas.

Katika hotuba yake ya mwaka mpya iliyowekwa kwenye Twitter, Rais Donald Trump alipongeza kati ya utengenezaji chanjo kama ”miujiza ya kimatibabu” na kupongeza juhudi za Operation Warp Speed, mpango wa Marekani unaolenga kutengeza na kuwasilisha chanjo.

Hata hivyo rais huyo hakuwataja kwa namna yoyote wamarekani karibu 350,000 waliofariki kutokana na corona.

Nchi za Asia-Pasifiki zimeathiriwa vipi?

Nchi ya kwanza inayokujia akilini ukitaja mwaka mpya ilikuwa Australia. Maonyesho ya fataki ya Sydney yalifanywa kama kawaida lakini watu hawakuruhusiwa kukusanyika kujionea kama ilivyo ada.

“Hatutaki kuwa na hafla ambayo itasambaza virusi mkesha wa mwaka mpya,” waziri mkuu wa New South Wales Gladys Berejiklian alisema.

Wakazi wengi wa Sydney walifuatilia onyesho hilo kwenye televisheni zao nyumbani, ambako watu watano tu waliruhusiwa kuwa pamoja.

China, tamasha la mwangaza linalofanyika kila mwaka katika mji mkuu wa Beijing lilifutiliwa mbali. Lakini katika mji wa Wuhan, ambao unadhaniwa kuwa chimbuko la janga la corona, maelfu ya watu walikusanyika katikati ya mji huo kusherehekea huku vibofu vikiachiliwa angani.

Japan ilifuta sherehe za jadi za kukaribisha mwaka mpya ambayo mfalme Naruhito na familia yake alikuwa awasalimie watu.

Nchini India, Delhi na miji mingine kadhaa, amri ya kutotoka nje usiku na masharti mengine ya kuzuia mikusanyiko mikubwa ya watu wakati wa mwaka mpya iliwekwa

Hata hivyo nchini New Zealand, ambako amri kali ya kutotoka nje na kufungwa kwa mipaka iliwekwa kumesaidia kuangamiza ugonjwa wa corona, sherehe za kuukaribisha mwaka maya ziliandaliwa kama kawaida.