NA MWAJUMA JUMA

MAKOCHA wa timu za soka za Simba na Yanga wamesema dakika 90 zitatoa bingwa wa kombe la mapinduzi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema wameingia katika fainali hiyo wana uhakika kuwa, utakuwa mchezo mgumu lakini bingwa lazima apatikane mwisho wa mchezo.

Kocha wa Simba Suleiman Matola alisema watahakikisha wanapambana ili kuibuka na ushindi.

“Nafikiri fainali ni fainali na hakuna fainali rahisi kama ambavyo watu wanafikiria, hasa ukiangalia zilikuwepo timu nyingi na zimebaki mbili haitakuwa mechi rahisi, lakini tutajipanga pamoja na ukubwa wa mechi hiyo ili tuhakikshe tunachukua ubingwa “, alisema.

Kwa upande wa kocha wa Yanga Cedric Kaze alisema fainali ni dakika 90 na wanajua kama kila mtu atajitoa ili aweze kushinda.

Hivyo alisema watafanya jitihada zao zote ili waweze kuondoka na ushindi na kutwaa ubingwa.

“Katika fainali hakuna kitu chengine cha kufanya isipokuwa unaenda kutafuta kombe na sisi tunajiandaa na kuwafanya wachezaji wapumzike ili wapate muda mzuri wa kujiandaa kwa mchezo huu”, alisema.

Timu hizo kwa mara ya miwisho walikutana katika michuano hiyo kucheza fainali mwaka 2011 na timu ya Simba ilishinda kwa mabao 2-0.

Mchezo wa fainali hiyo inatarajiwa kupigwa majira ya saa 2:00 usiku katika uwanja Amaan.