NA MWAJUMA JUMA

KITIMTIM cha ligi soka daraja la pili wilaya ya mjini kinazidi kupamba moto baada ya juzi kushuhudiwa miamba minne ikishuka katika viwanja vya Mao Zedong.

Miamba hiyo ni Baja ambayo ilishuka uwanja wa Mao Zedong A saa 7:30 kucheza na Shangani na ilishinda mabao 3-1, yaliyofungwa na Shaibu Said Othman ambae alifunga mawili na Salum Khamis na la Shangani lilifungwa na Nassor Khalifa.

Mnamo majira ya saa 10:00 uwanjani hapo kulikuwa na mchezo kati ya FC South na Negro United ambao ulimalizika kwa FC South kushinda bao 1-0.

Uwanja wa Mao Zedong B wakati wa saa 7:30 Union rangers na Nyerere Boys zilishindwa kutambiana kwa kufungana mabao 2-2, mabao ya Ranger yalifungwa na Abdalla Mohammed Said dakika ya 28 na Khatib Makame Juma dakika ya 59, wakati Nyerere Boy’s yote mawili yalifungwa na Abubakar Hassan Ali dakika ya 56 na 86.

Wakati wa Saa 10:00 timu ya ZFDC 2 ilitoka kidedea kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Urafiki, mabao ambayo yalifungwa na Fahmi Rajab dakika ya 33 na la pili urafiki walijifunga kupitia kwa mchezaji wao Ali Juma dakika ya 62 wakati akiokoa mpira uliopigwa na Nassir Abdalla.Bao lao hilo la kufutia machozi lilifungwa na Ibrahim Maulid dakika ya 44.

Ligi hiyo leo inatarajiwa kuendelea tena kwa kuchezwa michezo mitatu ambayo Kwaalinato United na Tanga City watacheza Mao Zedong A na Small Rangers na Colombia watakuwepo katika uwanja wa Mao Zedong B, huku Kwaalimsha na Negro FC watacheza katika dimba la Amaan, michezo yote itachezwa saa 7:30 mchana.