NA MWANDISHI WETU

MKUU wa wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja Sadifa Juma Khamis, amewahimiza wananchi wa wilaya hiyo kuendelea kudumisha amani na kuendeleza maridhiano ya kisiasa yaliyopelekea kuanzishwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Amesema hayo wakati alipopokea matembezi ya hiyari ya kuadhimisha miaka 57 ya mapindizi ya Zanzibar yaliyowashirikisha wanachama wa chama cha ACT Wazalendo na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kituo cha Walimu Mkwajuni, mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema matembezi hayo yanaonesha namna wanachama wa vyama hivyo na wananchi wanavyounga mkono uamuzi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kutekeleza matakwa ya katiba ya Zanzibar inayohitaji kuundwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye mfumo wa umoja wa kitaifa.

“Dk. Mwinyi (Hussein Ali Hassan) amemteua Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad katika nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na kuacha wazi baadhi ya wizara lakini pia ameteua Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar jambo ambalo linaimarisha umoja na mshikamano wa wananchi wa Zanzibar,” alieleza Sadifa.

Sadifa aliwaagiza viongozi wa dini wilayani humo kutumia majukwaa yao kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa mashirikiano, amani na kuvumiliana ili nchi iweze kufikia malengo ya maendeleo iliyojiwekea kwa haraka.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria matembezi hayo waliiomba serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wa vijijini ili watambue faida za kuwa na mfumo huo wa serikali ambao mbali ya Rais, una Makamu wawili wa Rais wanaotoka vyama tofauti.

Wamesema uzoefu unaonyesha kuwa serikali ya umoja wa kitaifa ya mwaka 2010 ilijikita kutoa elimu kwa viongozi juu ya kufanya mambo kwa pamoja huku wananchi walio wengi kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa mashirikiano ili nchi iweze kufikia maendeleo kwa haraka.

Maadhimisho ya miaka 57 ya mapinduzi ya zanzibar yalifikia kilele chake Januari 12, 2021 katika viwanja vya mnazi mmoja ambapo rais wa zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi dk. Hussein ali mwinyi na viongozi wengine alipokea maandamano ya wananchi na vikosi vya ulinzi na usalama.