NA HALIMA JUMA
MKUU wa Wilaya ya Chake Chake, Abdallah Rashid Ali amesema serikali imekusudia kuondoa matabaka, ili kujenga usawa kwa jamii. Aliyaeleza hayo ofisini kwake Chake Chake, wakati akizungumza na watendaji wa Wizara ya Afya kisiwani hapa.
Alifahamisha kuwa haipendezi kuona baadhi ya watumishi wanatumia vyeo au jina la mkubwa kufanikisha mahitaji yao kinyume na utaratibu. Aliwataka watumishi kuheshimu sheria na kanuni za
utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwa ni pamoja na utayari wa mtumishi kufanya kazi popote anapopangiwa.
“Fanyeni kazi kwa kufuata sheria na kanuni za utumishi wa umma wakati mnapotekeleza majukumu yenu, kwani mlipojaza mikataba mlikiri kufanya kazi sehemu yoyote ile,”alisema.
Alisema ni vyema wizara ya afya kuweka utaratibu wa
kusomesha watendaji wao ambao
hautoathiri shughuli za kawaida za utoaji huduma kwa
jamii.
Aliwataka wasimamazi wa vituo vya afya kutoa
huduma bora kwa wazazi ili kupunguza vifo vya mama na watoto.
Aidha alisema iwapo vituo vya afya vitawajibika ipasavyo, vitatoa fursa kwa hospitali kubwa kupunguza maradhi yanayosababishwa na mikusanyiko ya watu wengi.
Kwa upande wao madaktari walisema uhaba wa wafanyakazi,
vitendea
kazi ikiwemo dawa na vifaa tiba, mazingira
ambayo sio rafiki kwa kufanyia kazi,
ukosefu wa ada za kujilipia masomo, pamoja na ukosefu wa stahiki zao, ni mambo yanayowavunja moyo katika
utekelezaji wa majukumu yao.
Hivyo waliutaka uongozi wa wizara ya afya kupitia
katika hospitali na vituo vya afya, kwenda
kusikiliza changamoto za wafanyakazi.