NA MWANAJUMA MMANGA

MKUU wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Aboud Hassan Mwinyi, amesema atawachukulia hatua za kisheria madereva wa magari ya mchanga ambao wamekuwa wakikaidi maagizo yanayotolewa na serikali kuhusu uchimbaji  mchanga katika maeneo yasiyo rasmi kwa kisingizio cha kuuziwa maeneo hayo na wamiliki wa mashamba.

Alisema hivi karibuni alipofanya ziara katika maeneo yanayochimbwa mchanga kiholela na kuwakataza madereva hao kuacha tabia ya kuchimba mchanga katika maeneo yasiyo rasmi lakini bado wameonekana kukaidi maelekezo hayo hali ambayo inasababisha kutokea kwa uharibifu wa mazingira.

Akizungumza na madereva, wamiliki wa mashamba pamoja na wamiliki wa magari ya mchanga huko Mahonda, Aboud amesema  ili kuzuia vitendo hivyo ni vyema kwa wamiliki wa mashamba kuacha tabia ya kuuza maeneo yao bila ya kufuata taratibu zilizowekwa na serikali pamoja na kuahidi kufanya ziara za mara kwa mara katika maeneo yanayojihusisha na vitendo hivyo ili kulinda mazingira.

“Niwasihi sana wadereva wa mchanga iwapo mtu atakamatwa akifanya uharibifu wa uchimbaji kiholela basi sitomvumilia na hatua kali za kisheria nitamchukulia ikiwemo kulisimamisha ama kulifutisha uhalali wa ubebaji mchanga” alisema Mkuu huyo.

Hata hivyo, Aboud amewataka wachimbaji wa mchanga kuwa wastahamilivu kwani tayari serikali imeandaa eneo jengine na kilichobaki ni kuboresha miundombinu ya eneo hilo ili liweze kufanya kazi.

Mapema akitoa maelezo mbele ya Mkuu wa Wilaya Msimamizi wa Shimo la mchanga Pangatupu, Hassan Is-haka Bakar amewataka madereva hao kufuata taratibu za serikali ili kuzuia migogoro kwa wananchi.

Kwa upande wao wamiliki wa magari hao wamekiri kuhusika na uchimbaji wa mchanga kinyume na utaratibu na kuiomba serikali kufanya jitihada za haraka ili kufungua shimo jengine la mchanga kwani maisha yao yanategemea shughuli hiyo.

Kikao hicho kimefanyika baada ya kukamatwa kwa magari ya mchanga huko Bumbwini mafufuni siku ya Jumamaosi ambapo jumla ya madereva tisa  wamefikishwa katika kituo cha polisi Mahonda ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.