NA KHAMISUU ABDALLAH

KISANDUKU cha huduma ya kwanza kilichokosekana katika gari ya abiria, kimemsababishia dereva wa gari yenye namba za usajili Z 395 KS inayokwenda njia 511, kufikishwa mahakamani.

Gari hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Ali Bakar Ali (31) mkaazi wa Kijichi, wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mshitakiwa huyo alifikishwa katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe, mbele ya Hakimu Amina Mohammed Makame na kusomewa shitaka linalomkabili na Mwendesha Mashitaka, Koplo wa Polisi Salum Ali.

Ilidaiwa kuwa, mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la kuendesha gari ikiwa haina kisanduku cha huduma ya kwanza, kinyume na kifungu cha 51 (1) na 58 vya kanuni ndogo ya vyombo vya moto, sheria za Zanzibar.

Koplo Salum alidai kuwa, Januari 12 mwaka huu saa 2:45 asubuhi huko Malindi wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, mshitakiwa huyo akiwa dereva wa gari yenye namba Z 395 KS inayokwenda njia 511 akitokea Kinazini kuelekea Darajani, alipatikana akiendesha gari hiyo barabarani ikiwa haina kisanduku cha huduma ya kwanza, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alilikubali na kuiomba mahakama imsamehe kwa kudai kuwa hatorejea tena, huku upande wa mashitaka ukidai kuwa hauna kumbukumbu ya makosa ya zamani kwa mshitakiwa huyo mahakamani hapo, na kuomba kutolewa adhabu kwa mujibu wa shitaka alilopatikana nalo.

Mahakama ilimtia hatiani mshitakiwa huyo na kumuona ni mkosa kisheria na kumpa adhabu ya kulipa faini ya shilingi 40,000 na akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa mwezi mmoja. Mshitakiwa Ali aliahidi kulipa faini hiyo mbele ya mahakama, ili kujinusuru kwenda jela kwa muda huo