NA KHAMISUU ABDALLAH

DEREVA aliyedaiwa kuendesha chombo cha moto na kushindwa kubandika namba za usajili nyuma, amefikishwa katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe kujibu tuhuma hizo.

Mshitakiwa huyo ni Mohammed Abdalla Ali (42) mkaazi wa Mwera wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Akiwa katika mahakama ya Hakimu Amina Mohammed Makame, mshitakiwa huyo alisomewa shitaka linalomkabili na Mwendesha Mashitaka, Koplo wa Polisi Salum Ali.

Koplo Salum alidai kuwa, mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la kushindwa kubandika namba za usajili nyuma, kinyume na kifungu cha 31 (1) (4) cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.

Ilidaiwa kuwa Disemba 16 mwaka 2020 saa 3:30 asubuhi huko Mtofaani, mshitakiwa huyo akiwa dereva wa honda yenye namba za usajili Z 365 GF akitokea Welezo kuelekea Mwera, alipatikana akiwa anaendesha honda hiyo barabarani ikiwa hakuipachika namba za usajili nyuma, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alilikubali na kuiomba mahakama imsamehe, kwa kudai kuwa ndio kosa lake la mwanzo.

Upande wa mashitaka ulidai kuwa, pamoja na kutokuwa na kumbukumbu za makosa ya mshitakiwa huyo mahakamani hapo, adhabu itolewe kwa mujibu wa shitaka alilopatikana nalo.

Mahakama ilimtia hatiani mshitakiwa huyo na kumuona ni mkosa kisheria na kumpa adhabu ya kulipa faini ya shilingi 30,000 na akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi mitatu.

Mshitakiwa Mohammed alilipa faini hiyo ili kujinusuru kwenda Chuo cha Mafunzo.