NA NASRA MANZI

WANANCHI wa jimbo la Dimani wametakiwa  kuendelea kushirikiana katika harakati mbali mbali za kimaendeleo ikiwemo suala la usafi wa mazingira katika kituo cha afya ili kujipatia huduma bora.

Hayo yameelezwa na Mwakilishi wa jimbo la dimani Mwanaasha Juma Khamis, mara baada ya kufanya usafi wa mazingira na kutoa vifaa katika kituo cha Afya Kombeni Wilaya ya Magharibi B’ Unguja.

Alisema lengo la usafi kusherekea shamra shamra za kutimia  miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar,pamoja na kufanya usafi wa mazingira kwani ni jambo muhimu ambalo litasaidia kupatikana huduma bora kwa wananchi na kujikinga na maradhi mbalimbali.

Pia alisema ni vyema  kituo kuwa katika mazingira bora kutokana na huduma nyingi zinazotolewa kwa wananchi kutoka maeneo tofauti huwasili kwa ajili ya kupata huduma zinazotolewa na madaktari.

“Tumeungana na viongozi mbali mbali  ili kuweka kituo chetu cha afya katika hali ya usafi na kupata huduma bora kwani moja ya matunda ya Mapinduzi ni afya ,matibabu bure na elimu lakini pia kutoa vifaa “ alisema

Aidha alisema suala la usafi litakuwa endelevu kwa taratibu kwani wamejipanga ili kuona maeneo mengine ya jimbo la dimani kuwa katika ya mazingira mazuri.

Akizungumzia vifaa  vya kuwasaidia wagonjwa aliwataka madaktari hao kuvitumia kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa, ili kuona lengo la kuwasaidia wagonjwa linafikiwa.

Mbunge wa jimbo la Dimani Mustafa Mwinyi Kondo alisema wataendelea kushirikiana na wananchi wa jimbo hilo pamoja na madaktari ili kuona changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi kwa kila mwananchi anayefika kituo hicho kupatiwa huduma stahiki.

“Tumeshafanya ziara mbali mbali katika kituo na kufahamu changamoto za huduma lakini kuna mahitaji mengine hadi kufika katika serikali kuu,lakini changamoto ndogo ndogo kama viongozi tutashirikiana ili kuona ufanisi wa kituo unapatikana “ alisema

Ofisa Tabibu kituo cha afya Kombeni,  Abdulwahid Sadiq, aliwataka wananchi kudumisha usafi katika kituo hicho lakini pia kuwashajihisha wengine kutumia huduma za hospitali na kuacha dhana ya kujifungulia majumbani ili kuepusha matatizo.

Sheha wa shehia hiyo, Uledi Khamis, alisema wanakabiliwa na changamoto mbali mbali katika hospitali hiyo ikiwemo Ambulace kwa ajili ya kuchukulia wagonjwa,uhaba wa dawa, mashine kwa ajili kupatikana  maji  ndani ya kituo ,jambo ambalo linawalazimu kuingiza mpira ili kuepusha usumbufu kwa wagonjwa.