NA ASIA MWALIM

BARAZA la vijana Wilaya ya Magharibi ‘B’ limeatikiwa kushirikiana katika kuendeleza miradi inayoanzishwa, ili vijana waweze kujitegemea sambamba na kujiajiri.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Sera Uratibu na shughu za Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Dk. Khalid Salum Mohamed, aliyasema hayo alipokua akizindua kiwanda cha ushoni cha baraza la vijana huko Mchina mwisho Unguja.

Waziri huyo alisema, ipo miradi mbalimbali inayoanzishwa na vijana nchini inashindwa kuendelea kutokana na kukosekana uaminifu kati yao.

“Kuna miradi ya vikundi na ya watu binafsi inakufa kutokana na baadhi yao kufanya ujanja ujanja kwa wenzao” alisema.

Aidha aliwataka vijana hao kutokata tamaa pale wanapopatwa na tatizo la kazi na badala yake kubuni mbinu bora zitakazo kuza uchumi wao na taifa kiujumla.

Alifahamisha kuwa Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia uongozi wa Dk. Hussein Ali Mwinyi imelipa kipaombele suala la wajasiriamali kuwawezesha kielimu, kuwapa  mikopo na kuwapatia fursa za kimasomo. 

Aidha alitoa shukurani kwa Wizara ya Vijana, Habari, utamaduni na michezo kwa kuwapa mafunzo vijana hao sambamba na kuwapatia nyenzo muhimu za kujiendelezea ujuzi huo ikiwemo vyerehani 26.

Mapema Mkuu wa Wilaya mteule, Hamida Mussa Khamis, alisema vijana walioanzisha kiwanda hicho wataweza kuzalisha ajira mpya kwa vijana wengine.

Alieleza kuwa baraza la vijana Wilaya Magharibi ‘B’ limejipanga katika kuhakikisha vijana wa naondokana na  tegemezi kwa kujitafutia ajira binafsi bila kusubiri ajira kutoka serekalini.

Akisoma risala katika uzinduzi huo Katibu wa Baraza la Vijana Wilaya ya Magharibi ‘B’, Amina Mohammed Waziri, alisema vijana 20  waliopatiwa mafunzo wataweza kutoa mafunzo hayo kwa vijana wengine ili kuendeleza ujuzi huo .

Alieleza kuwa shughuli za ushoni zinazofanywa na vijana hao zimelenga kuimarisha kiwanda hicho sambamba na kupunguza tatizo la ajira nchini .

Alieleza malengo mengine ya baraza hilo ni kutoa msaada wa uniform kwa watoto yatima, wenye ulemavu,  pamoja na watoto wanaoishi katika mazingira magumu  Wilayani humo.

Sambamba na hayo alieleza changamoto zinazowakabili vijana hao ni eneo maalum kwa ajili ya shughuli za ushoni pamoja na upungufu wa vifaa ikiwemo meza, na kabati la kuhifadhia nguo.