NA MWANTANGA AME

HIVI Karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, katika kikao chake cha wadau wanaohusika na masuala ya udhalilishaji, ikiwa ni hatua ya kutafuta njia ya kupambana na tatizo hilo ambalo limesambaa kila kona ya nchi hii.

Dk. Mwinyi, akitoa hotuba yake katika kikao hicho alisema imefika wakati sasa kwa Zanzibar kuanzisha mahakama maalum ya makosa ya udhalilishaji, ili kupunguza mlolongo wa kesi katika mahakama. 

Alisema tayari ameshazungumza na Jaji mkuu na kukubaliana kimsingi kuanzisha mahakama hiyo, ambayo itatoa fursa ya kushughulikia kesi hizo na kufikia lengo la kuondoa malalamiko kwa wananchi.

Aidha alisema katika kulifanikisha hilo, watendaji wa taasisi zote zinazohusika na masuala ya kisheria wanapaswa kujitathmini juu ya utendaji wao na kufanya mabadiliko ya sheria kwa haraka ili kuweka sheria zitakazokidhi mahitaji.

Rais Mwinyi alisema tatizo la udhalilishaji ni kubwa na linaleta aibu katika nchi na maumivu makubwa kwa wananchi walio wengi na lisipokemewa kitaendelea kuharibu watoto.

Kimsingi mambo hayo mengi yakiwemo baadhi baadhi ya askari wasiowaadilifu kuwakejeli wanaowafanyia ukatili, udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia hali inayowaongezea madhara yakiwemo ya kisaikolojia na kiuchumi.

Mazingira ya ukusanyaji na utoaji wa ushahidi katika kesi hizo yanajatwa kama ni changamoto kubwa katika vita dhidi ya udhalilishaji, unyanyasaji na ukatili wa kijinsia hali inayohitaji kuwapo vyombo maalum vya kisheria  ikiwemo Mahakama kwa ajili ya masuala hayo.

Kama Jeshi la Polisi lilivyoanzisha Madawati  yanayowapa nafasi watoto yanayowahudumia na askari Polisi wenye mafunzo katika eneo hilo, ni wakati sasa baadhi ya watumishi wa Mahakama, Mahakimu na Majaji wakapata mafunzo maalum, ili wawe kwa ajili kushughulikia kesi hizo ambazo  pia zina changamoto nyingi.

Hii ni kwa kuwa mara nyingi waathirika wakubwa wa ukatili huu ni watu wanyonge katika jamii wakiwemo watoto wanawake wenye ulemavu na vikongwe.

Ndio maana ninasema kuundwa kwa Mahakama maluum ya vitendo vya udhalililishaji kutasaidia kuharakisha kesi za namna hiyo na haki itatendeka zaidi kwa kuwa watendaji wake watakuwa na mafunzo maalum kuhusu haki za binadamu na usawa wa kijinsia.

Naamini kuwapo kwa Mahakama hiyo kutapunguza kasi ya vitendo vya ubakaji, mimba za utotoni kwa wanafunzi, ulawiti vipigo vya mauaji kwa Imani za ushirikina.

Ndio maana ninasema umefika wakati watunga sera na sheria na mamlaka nyengine kuona huruma zaidi kwa waathirika na kulivalia njuga suala hili, ili lishiugulikiwe kwa nguvu maalum hali itayoleta ukombozi zaidi kwa jamii.

Ukombozi huu utapunguza ukatili huo na taifa lisipokuwa na watu waliofanyiwa ukatili litakuwa na watu wengi zaidi wasiotaka kufanyika kwa ukatili kwao na kwa wengine, ndio maana ninasema kama udhalilishaji unahitaji mahakama maalum.

Hivi sasa lipo tatizo la msingi linalohitaji ufumbuzi kwa kushirikiana pamoja ikiwemo serikali, wananchi, mahakama, Ofisi ya DPP, Jeshi la Polisi ikiwemo utoaji wa elimu kwa jamii ili kukinga tatizo hilo kabla halijatokea.

Aidha inatambua wapo wanaharakati, viongozi wa dini, masheha, waratibu na tasisi zisizo za kiserikali wanafanya kazi katika jamii, lakini tatizo bado linaendelea kuwepo hivyo imefika wakati kuchukuliwa hatua kali dhidi watu hao kwani ‘Anaeogopa uchungu hazai’ .