NA TALIB USSI
CHAMA cha ACT Wazalendo, kimepongeza hatua ya utiaji saini Mkataba wa Maelewano baina ya Oman na Serikali ya Zanzibar juu ya ujenzi wa Bandari Jumuishi huko Mangapwani, Kaskazini mwa Zanzibar
Katibu wa Idara ya Habari, Uenezi na Mahusiano Kwa Umma wa Chama Cha ACT Wazalendo, Salim Bimani amesema.”Hii ni hatua kubwa na muhimu kwa ajili ya uchumi na ukuaji wa Zanzibar inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Mwinyi.
Utiaji saini wa makubaliano hayo yaliyofanywa na Katibu Mkuu wa Wizara Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Amour Hamil Bakari, na kwa upande wa Oman alikuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji cha Oman Sheikh Mohammed Al-Tooqi ambaye aliongoza ujumbe kutoka Mamlaka hiyo.
Chini ya makubaliano hayo Oman imeweka nia kujenga bandari kadhaa kama vile ya mizigo na makontena, Petroli na gesi, Uvuvi na pia kuwepo chelezo kwa ajili ya matengenezo ya meli za ndani na nje katika ukanda huu, pamoja na kuweko eneo la viwanda, eneo la biashara na makaazi ya kisasa.
“Kila tukishikamana ndio tutaipa nguvu Serikali ya Umoja wa Kitaifa kufanya kazi na nchi mbali mbali na makampuni mbali. Tunaamini mazingira mazuri zaidi yatandikwa kushawishi wawekezaji zaidi,” alisema Bimani
Pia Bimani aliishukuru Serikali na watu wa Oman kudhihirisha uhusiano na udugu wa kweli kwa Zanzibar kwa kuweka nia ya mradi huo utakaotoa ajira kwa maelfu.