Ataka wakatatue changamoto za wananchi

NA KHAMISUU ABDALLAH

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wakuu wa wilaya aliowaapisha kufanya kazi kwa kujituma ili kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo jana mara baada ya kuwaapisha wakuu wa wilaya wapya aliowateuwa hivi karibuni hafla ilifanyika ikulu mjini Unguja.

Alisema sio wakati kwa wakuu hao kukaa ofisini na badala yake kushuka kwa wananchi kwani wanakabiliwa na changamoto mbalimbali na zinatakiwa kutatuliwa kwa haraka.

Dk. Mwinyi, alisema ni vyema kwa wakuu hao kufanya ziara za mara kwa mara na kusisitiza kwamba mkuu wa wilaya sio mtu wa kukaa ofisini na badala yake kuwa zaidi kwa wananchi.

Alisema kuna changamoto maalum ambazo zinataka kueka mkazo ikiwemo changamoto ya migogoro ya ardhi kwani kila siku wanapokea taarifa juu kuwepo kwa migogoro hiyo.

Jengine alisema ni usafi wa mji na masoko linalotokana na tatizo la Manispaa, lakini kama mkuu wa wilaya ana kila sababu ya kuhakikisha wilaya zao zinakuwa safi wakati wote kwani Zanzibar inatembelewa sana na watalii.

Agizo jengine kulivalia njuga suala la udhalilishaji wa kijinsia kwa watoto kwa kushirikiana pamoja kwa kuanza katika jamii na vyombo vyote vinavyohusika ili kuja na mpango mpya wa kushughulikia jambo hilo na kutafuta njia muafaka ya kuondosha vitendo hivyo nchini.

Eneo jengine alisema ni kuinua viwango vya elimu ndani ya wilaya zao ikiwemo kuhakikisha kwamba miundombinu, idadi ya walimu, vifaa vya kujifunzia na kufundishia vyote vinapatikana ili watoto waweze kupata elimu bora na kuinua kiwango cha elimu hapa Zanzibar.