NA LAILA KEIS

MATEMBEZI ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliyotembelea mabanda ya wajasiriamali walioshiriki katika maonesho ya bishara ya mapinduzi, yamewafurahisha wajasiriamali hao na kuona ni kiasi gani anavyowapa kipaombele.

Waliyasema hayo wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya Dk. Mwinyi alieambatana na mkewe mama Maryam mwinyi kumaliza ziara yake kwenye maonesho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Maisara mjini Unguja.

Walisema, katika maonesho mengi mara nyingi  viongozi hupendelea kutembelea mabanda ya Mawizara, ambapo kilikua ni kilio chao cha muda mrefu, hivyo ujio wa Rais umewapa matumaini na kuona ni namna gani anavyowapa kipaombele wajasiria mali wadogo wadogo.

Maryam Issa mjasiriamali kutoka kikundi cha ‘Kamba Refu’ wanaojishughulisha na utengezaji wa vitu vilivyofinyangwa kwa udongo, kama vile vyungu na birika alisema ujio wa Rais katika mabanda yao umewapa matumaini ya kuona ni kiasi gani anavyowajali.

“Nimefarijika sana kupata bahati ya kutembelewa na Rais katika banda langu, kwani huu ni mwaka wa tano tangu nishiriki haya maonesho, ambapo hapo nyuma nilikua nasikia tu kiongozi amekuja lakini sijawahi ata kuonana nae” alisema.

Aidha alisema kitendo hicho kinawazidisha imani wajasiriamali wadogo wadogo kuamini zile ahadi zake za tangu kampeni na baada ya kuapishwa kwake, za kusikiliza changamoto na kuwainua wajasiria mali hao anaanza kuzitimiza.

Asfar Mohamed mjasiria mali kutoka katika kikundi cha ‘Zenji Tamtam’ wanaouza vyakula vikavu na Ice cream alisema, ujio wa Rais katika mabanda yao umewafariji kwani matembezi kama hayo huwasaidia kutoa changamoto zao.

Nae Jeniffer James mjasiriamali kutoka katika kikundi cha ‘Mkaa Poa’ anaejishughulisha na utengezaji wa mkaa kutumia takataka, alimshukuru Rais kwa uamuzi wake wa kupita kuangalia biashara zao, ambapo walitamani ujio huo ili ajionee maendeleo ya wajasiria mali hao.

“Huu ni mwaka wangu wa saba kushiriki maonesho haya ya mapinduzi, nilikua nikitamani japo mara moja kiongozi apite angalau karibu na banda langu, kiukweli nimefarijika sana” alisema.

Alisema hiyo inaonesha kwa vitendo ni kiasi gani Rais anavyowajali na kuwapa kipaombele wajasiriamali.

Maonesho hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya viwanda Zanzibar, ni moja ya shamrashamra ya maadhimisho ya  Mapinduzi, ambayo   yameyopokea muamko mkubwa zaidi kwa wajasiriamali, wafanyabiashara na wananchi wa ndani na nje ya visiwa vya Zanzibar.