NA MWANAJUMA MMANGA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa kimataifa unaohusiana na masuala ya wazee unatarajiwa kufanyika Januari 18, mwaka huu katika hoteli ya Verde, Mtoni Zanzibar.

Katibu wa Jumuiya ya Wazee Zanzibar (JUWAZA II) Amani Suleiman Kombo, aliyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili huko ofisini kwao Amani, Unguja.

Alisema mkutano huo umeandaliwa na Shirika linalosaidia wazee Duniani Help Age International, kikawaida hufanyika katika nchi tofauti kila mwaka, una lengo la kuangalia masuala ya wazee na changamoto zinazowakabili.

“Hii ni fursa kwa nchi yetu kuonesha namna inavyowajali wazee, kwani mbali ya wanachama kutoka nchi mbali mbali Afrika na mashirika ya kimataifa, Mtendaji mkuu wa Helpage International, Smat Daniel na timu yake atakuwepo,” alieleza Kombo.

Alisema masuala ya wazee kitaifa na kimataifa ikiwemo kuwajengea nyumba zao, kuwapatia matunzo na huduma za kijamii  zimeimarika nchini na kuifanya zanzibar kuwa ya kwanzo iliyoanzisha mfumo rasmi wa matunzo ya wazee na kuwa mfano Afrika.

 Aliongeza kuwa mkutano huo wa siku saba, utajadili mada mbali mbali zinazohusu ustawi na hifadhi ya wazee na kwamba Zaidi ya washiriki 80 kutoka nchi za Uganda, Ethiopia, Zimbabwe, Malawi, Kenya, Uholanzi na nchi nyengine za Ulaya na Marekani.

“Kuja kwa wageni hawa hapa Zanzibar sio kutatoa nafasi ya kutangaza mafanikio ya nchi yetu pekee, kutaingiza mapato,” alisema Kombo.

Aliongeza kuwa Zanzibar itaandika historia kwa mara ya kwanza kufanyika mkutano huo nchini na kueleza kuwa jumuiya hiyo ina imani Dr. Hussein Mwinyi ni mweledi na mchapakazi katika kuwasaidia wazee wakati alipokuwa mbunge wa jimbo la Kwahani kwani wazee waliweza kutoa mchango wao mkubwa wakati wa ujana wao.

Aidha aliwaomba wafanyabiashara wa hoteli za kitalii, taasisi, mashirika na wananchi zinazosimamia fedha kutoa mashirikiano kwa wageni hao kuwa wakarimu ili Zanzibar iendelee kupata sifa.