LONDON,UINGEREZA

DUNIA imepoteza zaidi ya hekta milioni 43 ya misitu katika kipindi cha muongo mmoja uliopita kufuatia uharibifu wa baadhi ya misitu.

Hayo ni kulingana na shirika la kimataifa la kuhifadhi aina mbalimbali ya mimea na wanyama WWF.

Tathmini iliyofanywa na WWF ilibaini kwamba uharibifu uliofanyika katika misitu 29 Marekani ya Kusini, barani Afrika na kusini mashariki mwa Asia, ulisababisha nusu ya idadi jumla ya hekari za misitu iliyoangamia duniani kote.

Shirika la WWF limesema tathmini hiyo ilijikita kwenye picha za satelaiti zilizorikodiwa kati ya mwaka 2004 na 2018 katika maeneo 24 yenye hatari zaidi kwa uharibifu wa misitu duniani. Kila mwaka hekta nyingi za misitu huharibiwa haswa kuwezesha kilimo kwa kiwango kikubwa,huku maeneo yenye utajiri wa viumbe mbalimbali yakibadilishwa kuwa sehemu za malisho kwa mifugo na upanzi wa mimea.

Uharibifu mkubwa ulifanyika katika msitu wa mvua wa Amazon nchini Brazil, Colombia, Peru, Bolivia, Venezuela na Guyana ambapo hekari milioni 18.2 za misitu iliteketea moto.