KAMPALA,UGANDA
TUME ya Uchaguzi (EC) imemzuia mgombea wa urais Robert Kyagulanyi, anayejulikana kama Bobi Wine, kufanya kampeni katika wilaya 16 bila ruhusa.
Bobi Wine alikuwa na matumaini ya kurudi katika wilaya alizoruka ratiba yake ya kampeni lakini EC inamtaka asaini mkataba wa makubaliano (MoU) kabla ya kuanza safari ya kurudi wilayani.
Bobi Wine alikataa sharti hilo, akisema wagombea wengine wa urais wako uwanjani wakifanya kampeni bila kusaini waraka huo.
Daily Monitor haikuweza kuthibitisha ikiwa wagombea wengine wa urais walitia saini MoU au la.
Baadhi ya wilaya zinazohusika ni Kaliro, Pallisa, Kaberamaido, Kwania, Namutumba, Ngora, Bukedea, Kalaki, Amolatar, Serere, Buyende, Bugweri, Butebo na Dokolo.
Katika MoU, wagombea wote wa urais wanahitajika kufanya kampeni za amani, kufuata miongozo ya Covid-19 kutoka kwa miongozo ya Wizara ya Afya na EC juu ya maandamano.
Bobi Wine alisema amekosa kufanya kampeni katika wilaya hizi kwa sababu polisi walimzuia kufikia maeneo haya bila ufafanuzi.
Msemaji wa EC Paul Bukenya alimkumbusha Bobi Wine kwamba hakuwa na njia nyengine ila kufuata masharti yaliyowekwa kabla ya kutembelea wilaya hizo 16.
Wiki iliyopita, ikitoa mfano wa kuongezeka kwa maambukizo ya Covid-19 na ukiukaji wa taratibu za kawaida za wagombea, EC ilisitisha mikutano ya kampeni huko Wakiso, Kampala, Mbarara, Kabarole, Luweero, Kasese, Masaka, Wakiso, Kabarole, Jinja, Kalungu, Kazo, na Tororo.